Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Ni Mwisho wa Manabii na Mitume).
Na baada ya kunyanyuliwa Issa -Amani iwe juu yake- kilipita kipindi kirefu takribani karne sita (miaka mia) (600) watu wakazidi kupotoka na kuacha uongofu, na ukawaenea Ukafiri na upotofu na kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Basi Mwenyezi Mungu akamtuma Muhammad – rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- katika mji wa Makka katika ardhi ya Hijjazi kwa uongofu na dini ya haki; ili amuabudu Mwenyezi Mungu mmoja tu, na akamzawadia alama na miujiza mbali mbali yenye kujulisha juu ya utume wake na ujumbe wake na akawa kwa ujumbe huo ni mwisho wa mitume, na akaifanya dini yake kuwa ndiyo mwisho wa dini zote na akaihifadhi na kutobadilishwa na kugeuzwa mpaka mwisho wa maisha ya dunia na kusimama kiama, Basi ni nani huyo Muhammadi?
Na, ni akina nani watu wake?
Na ni vipi alimtuma?
Ni ipi Dalili ya Utume wake?
Na ni upi ufafanuzi wa historia yake?
Haya ndiyo tutakayojaribu kuyaweka wazi kwa idhini ya Allah katika kurasa hizi za muhutasari.
A- Nasaba (ukoo) wake na Utukufu wake .
Yeye ni Muhammad bin Abdillahi, mtoto wa Abdulmuttwalib mtoto wa Haashim Mtoto wa Abdi Manafi, mtoto wa Qusswayyi, mtoto wa Kilabi, Nasaba yake inafika kwa Ismail Mtoto wa Ibrahim -juu ya wawili hao amani- ni katika kabila la Makuraishi wanaotokana na waarabu, alizaliwa Makkah mwaka 571 tangu kuzaliwa kwa Masiha -Amani iwe juu yake-
Alifariki baba yake mzazi hali yakuwa yuko tumboni kwa mama yake na akaishi hali yakuwa ni yatima na akalelewa na Babu yake Mzee Abdulmuttwalib, kisha baada ya kufa babu yake alilelewa na baba yake mdogo aitwae Abuu Twaalib.
B- Sifa zake:
Tumetaja kuwa Mtume mteuliwa anatoka kwa Mwenyezi Mungu ni lazima awe ni katika kilele cha juu kutoka katika nafsi yenye kuheshimika na mwenye maneno ya kweli na tabia njema na vile vile alikuwa Muhammad -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- kwa hakika aliishi hali yakuwa ni mkweli muaminifu mwenye tabia njema mwenye maneno mazuri mwenye ulimi fasaha na mwenye kupendwa na watu wa karibu pia na wa mbali akitukuzwa na watu wake akiheshimiwa kati yao, na walikuwa hawamuiti isipokuwa kwa jina la muamunifu, na walikuwa wakitunza kwake amana zao wakati wanaposafiri.
Na kwa kuongezea uzuri wa tabia zake; kwa hakika alikuwa ni mzuri wa umbile jicho halichoki kumwangalia, mwenye uso mweupe mwenye macho makubwa mwenye nyusi nyingi, mwenye nywele nyeusi, na mabega mapana, hakuwa mrefu sana wala mfupi na alikuwa mwenye kimo cha kati na kati na alikuwa anakaribia urefu. Na anamsifia mmoja kati ya maswahaba zake kwa kusema:
“Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- akiwa katika pambo (vazi) la kiyemeni sijawahi kumuona mtu mzuri kama yeye”
Na alikuwa hawezi kusoma wala kuandika tena akiwa amezungukwa na watu wasiojua kusoma wala kuandika na ni Nadra sana kumpata mmoja wao mwenye kuweza kusoma na kuandika lakini walikuwa ni wajanja na wenye nguvu na kumbukumbu za haraka pasina kufikiria.
C- Makuraish na Waarabu.
Walikuwa ni Watu wa Mtume – Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na Jamaa zake wa karibu wakiishi katika mji wa Makkah pembeni mwa nyumba tukufu na Al-kaaba tukufu ambayo Mwenyezi Mungu alimuamrisha Ibrahimu- juu yake amani aijenge yeye na mwanaye Ismail.
Lakini baada ya kupita muda mrefu waliachana na dini ya Ibrahim (kumtakasia dini Mwenyezi Mungu) na wakaweka wao- na makabila yaliyokuwa yanawazunguka- masanamu yatokanayo na mawe na miti na dhahabu pembeni mwa Al-kaaba, na wakayatukuza na wakaitakidi kuwa yanauwezo wa kunufaisha na kudhuru na wakaanzisha utaratibu wa kuyaabudu, na masanamu yaliyokuwa maarufu zaidi ni sanamu linaloitwa Hubal, ambalo lilikuwa ni sanamu kubwa na lenye mambo makubwa.
Ukiongezea masanamu wengine na miti iliyoko nje ya Makka iliyokuwa ikiabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu, na huzungushiwa mapambo ya utakatifu, na yalikuwa maisha yao yamezungukwa na mazingira ambayo pembezoni mwake kumejaa upingaji haki, ufahari na kiburi na kuwafanyia uadui wengine na vita vikali, japokuwa palikuwepo kati yao wenye tabia nzuri mfano ushujaa na kuwakirimu wageni na ukweli wa maneno na mambo mengine.
Kutumwa kwa Mtume Rehema na amani za Allah ziwe juu yake anasema:
Na alipo fikisha Mtume-Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- miaka arobaini na alikuwa katika pango la Hiraa nje kidogo ya mji wa Makkah, ulimshukia Wahyi wa kwanza kutoka mbinguni kutoka kwa Mwenyezi Mungu basi akamjia Malaika Jibrili, akambana na akamwambia, Soma, akasema : Mimi siyo msomaji kisha akambana mara ya pili mpaka akachoka kwa kubanwa ,akasema kwa kumwambia, soma, akasema Mimi siyo msomaji, kisha akambana mara ya tatu mpaka akachoka zaidi kwa kubanwa kisha akamwambia: Soma, akamuuliza nisome nini, akasema:
Soma, ewe Nabii, Qur’ani uliyoteremshiwa ukianza kwa Jina la Mola wako Aliyepwekeka kwa kuumba.
Aliyemuumba kila binadamu kwa pande la damu nzito nyekundu.
“Soma, ewe Nabii, kile ulichoteremshiwa, na Mola wako ni Mwingi wa wema, Mwingi wa ukarimu”.
Aliyewafundisha viumbe wake kuandika kwa kalamu.
Alimfundisha binadamu vitu ambavyo hakuwa akivijua. Akamtoa kwenye giza la ujinga, Akampeleka kwenye nuru ya elimu.
[Surat Al-alaq]
Kisha akaondoka Malaika na akamuacha, basi akarudi Mtume-Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- nyumbani kwake kwa mkewe akiwa na khofu ya hali ya juu, na akamwambia mkewe Khadija nifunike mimi naogopa, mke wake akamwambia, siyo hivyo na hatokufedhehesha Mwenyezi hata mara moja, kwa hakika wewe utaunga udugu na utabeba matatizo na utawasaidia watu katika matatizo makubwa.
Kisha akamjia Jibrili akiwa kwenye sura yake ambayo Mwenyezi Mungu amemuumbia, akiwa amefunika vilivyomo mpaka mwisho mwa upeo wa macho, akasema: ewe Muhammad mimi ni Jibrili na wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Kisha ukafululiza Wahyi kutoka mbinguni ukimuamrisha Mtume kuwalingania watu wake kwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuwatahadharisha na ushirikina na ukafiri, na akaanza kuwalingania watu wake mmoja mmoja na watu wake wa karibu; ili kuwaingiza katika uislamu na wa kwanza kuuamini ni mke wake Khadija bint ya Khuwailid na Rafiki yake kipenzi Abuu bakar aliye mkweli na mtoto wa baba yake mdogo ambaye ni Ally mtoto wa Abuu twaalib.
Kisha baada ya kujua watu wake kuwa anawalingania walianza kumpiga vita na kumfanyia vitimbi na uadui. Alitoka kwa watu wake asubuhi ya siku moja na akawaita kwa sauti yake ya juu “Waa swabaahaau” Ni neno wanalolisema waarabu wanapotaka kuwakusanya watu, (kama kusema: kumekucha! kumekucha! La mgambo likilia kuna jambo) basi wakamfuata watu wake wakikusanyika ili kusikia wanaambiwa nini, na walipojikusanya akawaambia: “Hivi mnaonaje ikiwa nitawapa habari kuwa maadui wamekuvamieni asubuhi au jioni hivi mtakuwa ni wenye kunisadikisha? wakasema, haijawahi kutokea wewe kusema uongo akasema: basi mimi kwenu nyinyi ni muonyaji wenu kuhusu adhabu kali. Kisha baba yake mdogo Abuu Lahab naye ni mmoja kati ya baba zake wadogo, na yeye na mke wake ndiyo walikwa wenye uadui mkubwa na Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- ‘Umepata hasara wewe! hivi umetukusanya kwa jambo hili? basi akateremsha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake – Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“Imehasirika mikono miwili ya Abu Lahab, na yeye mwenyewe ameangamia, kwa kumuudhi Mtume, rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani. Hasara ya Abu Lahab ilithubutu.
Haikumfaa mali yake wala alichokichuma
Ataingia kwenye Moto wenye miale,
yeye na mke wake ambaye alikuwa akibeba miba na kuiweka kwenye njia anayopita Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ili kumuudhi.
Kwenye shingo yake patakuwa na kamba imara gumu ililio kavu, atabebwa nayo kwenye Moto wa Jahanamu, kisha atarushwa nayo mpaka chini.
[Surat Al-masad 1-5]
Kisha akaendelea Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- akiwalingania katika uislamu, na akiwaambia semeni Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee, mkisema hivyo mtafaulu, wakasema, hivi umeifanya miungu kuwa Mungu mmoja hakika hili ni jambo la ajabu mno.
Na zikashuka aya mbali mbali kutoka kwa Mwenyezi Mungu zikiwalingania kwenye uongofu na zikiwatahadharisha na upotovu ambao walikuwa nao, miongoni mwa hizo Aya ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
“Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina kwa kuwakaripia na kulionea ajabu tendo lao, «Je nyinyi mnamkanusha Mwenyezi Mungu Aliyeumba ardhi kwa siku mbili, mnamfanya kuwa Ana washirika na wanaofanana Naye mkawa mnawaabudu pamoja Naye? Muumbaji Huyo Ndiye Mola wa viumbe wote.
«Na Akajaalia Mwenye kutakasika katika ardhi majabali yaliyojikita juu yake, Akaibarikia kwa kuifanya iwe na kheri nyingi kwa watu wake, Akakadiria humo riziki za chakula kwa watu wake na yale yanayowafaa maishani kwa kipindi cha Siku nne: Siku mbili Aliumba ndani yake ardhi na Siku mbili Aliweka katika ardhi majabali yaliyojikita na Akakadiria katika Siku mbili hizo riziki zake zikiwa sawa kwa wenye kuuliza, yaani kwa mwenye kutaka kuliuliza hilo apate kulijua.
Kisha Akalingana sawa mbinguni, na ilikuwa moshi hapo kabla, Akasema kuiambia mbingu na ardhi, «Fuateni amri yangu kwa hiari au kwa nguvu!» Nazo zikasema, «Tumekuja tukiwa watiifu kwako. Hatuna matakwa kinyume cha matakwa yako.»
Mwenyezi Mungu Akapitisha kuziumba mbingu saba na kuzisawazisha kwa Siku mbili. Na kwa hilo ukatimia uumbaji wa mbingu na ardhi kwa Siku sita kwa hekima Anayoijua Mwenyezi Mungu, pamoja na uweza Wake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, wa kuziumba kwa mara moja. Na Akapeleka wahyi katika kila mbingu kwa Analolitaka na kuliamuru. Na tumeipamba mbingu ya karibu kwa nyota zinazong’ara na kwa ajili ya kuuhifadhi na Mashetani wanaosikiliza kwa kuiba. Uumbaji huo mzuri ni makadirio ya Aliye Mshindi katika ufalme Wake, Aliye Mjuzi Ambaye ujuzi Wake umekizunguka kila kitu.
Basi wakipuuza wakanushaji hawa baada ya kubainishiwa sifa za Qur’ani zinazotajika vyema, na sifa za Mungu Mkubwa, waambie, «Kwa kweli, ninawaonya nyinyi adhabu yenye kuwamaliza mfano wa adhabu (iliyowashukia watu wa kabila la) ‘Ād na Thamud walipomkanusha Mola wao na kuwaasi Mitume wao.»
[Surat Fuswilat 9-13]
Lakini aya hizi na kule kulinganiwa hakukuwazidishia isipokuwa kuzidisha maasi na kuwa na kiburi cha kuiacha haki, bali wakazidi kuwaadhibu kila mwenye kuingia katika dini ya uislamu, na haswa wale wanyonge ambao hawana watu wa kuwakingia kifua, basi wakawa wanaweka katika kifua cha mmoja wao jiwe kubwa, wanamkokota kumpitisha masokoni katika wakati wa jua kali na wakimwambia kufuru dini ya Muhammad au ridhika na adhabu hii, mpaka wako miongoni mwao walikufa kutokana na adhabu hii kali.
Ama Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- alikuwa kwenye himaya ya baba yake mdogo Abuu twaalib ambaye alikuwa akimpenda na akimuhurumia na alikuwa ni katika wakubwa wa kabila la kikuraishi lenye kuogopwa, isipokuwa hakuingia katika uislamu.
Na wakajaribu Makuraishi kumjadili Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- juu ya Da’wa yake wakamuahidi mali na ufalme na vyenye kudanganya ili aachane na kulingania katika dini hii mpya ambayo inafanya kuonekana wabaya miungu wao ambayo wanaitukuza na kuiabudu kinyume na Mwenyezi Mungu, na ukawa msimamo wa Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- ni mkali wenye kukatisha tamaa, kwa sababu jambo hili ni amri ameamrishwa na Mwenyezi Mungu ili alifikishe kwa watu, na kama ataachana na jambo hili basi atamuadhibu Mwenyezi Mungu.
Na akawaambia kuwa mimi nawatakia khere na nyinyi ni watu wangu na jamaa zangu
“Na ninamuapa Mwenyezi Mungu lau kama ningewadanganya watu wote basi nisingekudanganyeni nyinyi, na lau kama ningewafanyia hiyana watu wote basi nisingekufanyieni nyinyi”.
Na walipoona kuwa juhudi za kujadiliana naye hazikufanikiwa katika kusimamisha Da’awa, uadui wa makuraishi ukazidi dhidi ya Mtume-Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na wafuasi wake. Na wakataka makuraishi kutoka kwa Abuu twaalib amsalimishe Muhammad -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- ili wamuue, na wampe wakitakacho au aache kuieneza dini yake kati yao, basi Baba yake mdogo akamtaka ajizuie kuilingania dini hii.
Basi akaelezea Mtume -Rehema za mwenyezi mungu ziwe juu yake na amani- na akasema:
“Ewe Baba yangu Mdogo, namuapia Mwenyezi Mungu, lau wangeweka jua katika mkono wangu wa kulia na wakaweka Mwezi upande wangu wa kushoto ili niiache dini hii, sitoweza kuiwacha dini hii mpaka Mwenyezi Mungu aidhihirishe dini hii au nife kwa ajili yake .
Basi akasema Baba yake mdogo: Nenda na useme lile utakalo kulisema na hawatakufanya chochote na wakikufanya chochote niko tayari kufa kwa ajili yako, na yalipomfika Abuu twalib mauti na mbele yake kulikuwa na baadhi ya wakubwa wa kikuraishi alimjia Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- akimsisitiza kuingia katika uislamu na akimwambia: Ewe Baba yangu mdogo sema Neno ambalo nitakudhamini kwalo mbele ya Mwenyezi Mungu, sema: ‘Laa ilaaha illa llahu’ basi wakubwa wakamwambia, hivi unataka kuiacha mila ya Abdul mutwalib (yaani unaiacha dini ya mababa na mababu) basi akaona ni jambo kubwa sana kuiacha dini ya baba zake na kuingia katika dini ya uislamu hivyo akafa hali yakuwa ni mshirikina.
Basi akahuzunika Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- huzuni iliyokuwa kubwa kwa kufa Baba yake mdogo katika ushirikina, basi Mwenyezi Mungu akampa habari kwa kauli yake:
“Hakika Wewe, ewe Mtume, humuongoi, unayependa aongoke. Lakini hilo liko kwenye mkono wa Mwenyezi Mungu, Anamuongoa Anayemtaka kumuongoa kwenye Imani na kumuafikia aifuate. Na Yeye Ndiye Anayemjua zaidi anayefaa kuongoka, hivyo basi Anamuongoa”.
[Suratil Qaswas 56]
Na alipata maudhi Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- baada ya kufa Baba yake mdogo Abuu Twaalib na wakawa wanachukua uchafu (kinyesi cha wanyama) na wakimuwekea mgongoni mwake wakati akisali mbele ya Kaaba.
Kisha akatoka Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- kuelekea mji wa Twaif ili awalinganie watu wa Twaaif kuingia katika uislamu, (nao ni mji wenye umbali wa kilo mita 70 kutoka katika mji wa Makkah) wakaipinga Da’awa yake vikali kuliko walivyoipinga watu wa Makkah, na wakawashawishi wale wapuuzi wao kwa kumpiga Mtume mawe -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na wakamfukuza kutoka Twaif na wakawa wanamfuatilia nyuma wakimrushia mawe mpaka wakamtoa damu kwenye visigino vyake vitukufu.
Basi akaelekea Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- kwa Mola wake akimuomba na kumtaka amnusuru, basi Mwenyezi Mungu akamtumia Malaika akamwambia, “Hakika Mola wako amesikia namna wanavyokusema watu wako, sasa ikiwa utataka nitawabananisha kwa milima miwili- yaani milima miwili mikubwa-” Akasema Mtume: Hapana lakini natarajia kwa Mwenyezi Mungu kuwa atatoa katika migongo yao wenye kumuabudu yeye peke yake na wala hawatomshirikisha na chochote.
Kisha akarudi Makkah Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na uadui ukaendelea na mashambulizi kutoka kwa watu wake kwa kila aliyemuamini alifanyiwa uadui, kisha likaja kundi kutoka katika mji wa Yathriba – mji ambao baada ya hapo ukaitwa kwa jina la Madinah- wakaja kwa Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- akawalingania katika uislamu nao wakasilimu, na akawatumia mmoja wa maswahaba zake akiitwa Mus’abu mtoto wa Umair akiwafundisha mafundisho ya uislamu, na wakasilimu kwenye mikono yake watu wengi wa Madina.
Na wakaja kwa Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- mwaka uliofuata wakimpa ahadi ya utiifu katika kuingia kwenye uislamu, kisha akawaamrisha maswahaba zake kuhamia Madina na wakahama makundi kwa makundi na mtu mmoja mmoja -na wakapewa jina la Muhaajiriina – (Yaani: Wahamiaji) na wakawapokea watu wa Madina kwa ukarimu na ukaribisho mzuri na kwa kuwakubali na wakawakaribisha katika majumba yao na wakagawana nao mali na majumba yao- na wakaitwa baada ya hapo kuwa ni Answar- (Watetezi)
kisha Makuraishi walipojua kuhama huku wakakubaliana kumuua Mtume -Rehema za mwenyezi mungu ziwe juu yake na amani-, na wakakubaliana waivamie nyumba yake ambayo analala humo, na akitoka wampige na upanga pigo kama la mtu moja, Mwenyezi Mungu akamuepusha nao na akawatoka pasina wao kuhisi chochote, na akakutana na Abuu bakar Swiddiq na akamuamrisha Ally kubakia Makkah ili aweze kurudisha amana za watu zilizohifadhiwa kwa Mtume kwa wenyenazo.
Na akiwa njiani anahama Makuraishi waliweka zawadi yenye thamani kubwa kwa yeyote atakaye mkamata Muhammad -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- sawa awe hai au amekufa, lakini Mwenyezi Mungu akamuokoa nao akafika Madina na swahiba wake Abuubakar wakiwa salama .
Na wakampokea watu wa Madina kwa bashasha na ukaribisho mzuri na furaha ya hali ya juu, na wakatoka wote kwenda kumpokea Mtume wa Mwenyezi Mungu wakisema amekuja Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Yalidumu Makazi kwa Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani-, na akaanza kujenga msikiti kwanza ili kusimamshwe humo sala, kisha akawa anawafundisha watu sheria za uislamu na akiwasomea Qur’ani na akiwalea kwa tabia njema, wakakusanyika pembeni mwake maswahaba zake wakijifunza toka kwake uongofu na wakatakasika nafsi zao kutokana na uongofu na tabia zao zikawa za hali ya juu na mapenzi yao ya kumpenda Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- yakawa ni ya ndani na wakaathirika na sifa zake za hali ya juu na mafungamano ya udugu wakiimani yakawa ni yenye nguvu.
Na ukawa mji wa Madina ni mji wa Madina kweli kweli wenye kupigiwa mfano, Madina ambayo unaishi katika anga iliyojaa furaha na udugu, hakuna tofauti kati ya tajiri wala masikini wala mweupe na mweusi wala hakuna tofauti kati ya mwarabu na asiyekuwa mwarabu wala hawajioni bora baadhi yao kwa wengine isipokuwa kwa imani na uchamungu, na likatengenezeka kwa watu hawa wateule Taifa bora na la ukweli lililokuwa na likajulikana kihistoria.
Na baada ya mwaka mmoja kuanzia alipohama Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- yalianza mashambulizi na vita kati ya Mtume na maswahaba zake dhidi ya kabila la kikuraishi, na kila aliyekwenda pamoja na kabila hilo katika kuifanyia uadui dini ya uislamu.
Na vikatokea vita vya kwanza kati yao, navyo ni vita vya Badri vikubwa katika bonde lililopo kati ya Makkah na Madina, akawapa Mwenyezi Mungu msaada waislamu, na walikuwa idadi yao ni wapiganaji 314 wakipigana na Makuraishi ambao idadi ya wapiganaji wao walikuwa 1000, na waislamu wakapata ushindi wa kutosha, na wakauliwa Makuraishi sabini na wengi wao ni wakubwa na viongozi wa Makuraishi, na waliobakia wakakimbia.
Kisha zikaja vita vingine kati ya Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na Makuraishi, aliweza Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- katika mwisho wake (Baada ya kurudi kwake toka Makkah kwa miaka minane) kulipeleka jeshi ambalo nguvu yake ilikuwa ni wapiganaji 10,000 miongoni mwao ni katika walioingia katika uislamu walipokuwa Makka tukufu ili kuwapiga vita Makuraishi nyumbani kwao na waingie mji wa Makkah kwa nguvu na waweze kuwashinda ushindi wenye nguvu, na kulishinda kabila lake ambalo lilitaka kumuua na kuwaadhibu maswahaba zake na likazuia watu kuingia katika dini ambayo amekuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Basi akawakusanya baada ya ushindi uliokuwa mashuhuri na akasema kuwaambia:
Enyi kundi la Kikuraishi Hivi mnadhani kuwa mimi nitawafanya nini?wakasema: Ndugu mkarimu na mtoto wa ndugu yetu mkarimu, akasema: Basi ondokeni kwani nyie mko huru, akawasamehe na akawapa uhuru wa kujiiunga na dini ya uislamu”.
Na ikawa hii ni sababu ya kuingia watu katika dini ya uislamu makundi kwa makundi, na likasilimu bara arabu lote na wakaingia katika dini ya uislamu.
Na wala haukupita muda mrefu akawa amehiji Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na wakahiji pamoja naye watu 144,000 katika wale wapya waliongia katika dini ya uislamu.
Na akasimama akiwahutubia katika siku ya Hijja kubwa na akiwabainishia hukumu za dini na sheria za uislamu kisha akawaambia: “Huenda mimi na nyie tusikutane tena baada ya mwaka huu, basi fahamuni kuwa inatakiwa amfikishie aliyekuwepo yule asiyekuwepo”. Kisha akawaangalia na akasema: “je nimefikisha?” Watu wakasema: ndiyo, akasema: “Ewe Mola wangu wa haki shuhudia”. Akasema: “Tambueni kuwa nimefikisha” Watu wakasema: ‘ndiyo’ Akasema: “Ewe Mola wangu shuhudia kuwa nimefikisha”.
Kisha akarudi Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- katika mji wa Madina baada ya Hijja, na akawahutubia watu siku moja na akawaambia; “Hakika mja amepewa hiyari na Mwenyezi Mungu kati ya kubakia duniani au kuchagua yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu basi mja akachagua yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu”, wakalia maswahaba na wakawa wamejua kuwa yeye anakusudia nafsi yake na kuwa yeye yuko karibu kufariki na kuiacha dunia, na katika siku ya juma tatu ya tarehe kumi na mbili mwezi wa tatu Hijiria katika mwaka wa kumi na moja tangu kuhama Mtume, yalizidi maradhi ya bwana Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na kikamuanza kilevi cha mauti, akawatazama maswahaba wake mtazamo wa kuwaaga na akawausia kuzihifadhi sala na akaisalimisha roho yake tukufu na akahama kuelekea kwa kipenzi aliye juu.
Walipata pigo maswahaba -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- na wakapata huzuni na masikitiko makubwa na msiba ukawaathiri mpaka ikafikia hatua mmoja wao ambaye ni Omari bin khatwab -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- alisimama akiwa amechomoa upanga wake kutokana na mfadhaiko mkubwa na akasema: sitosikia yeyote anasema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amekufa isipokuwa nitamuua.
Basi akasimama Abuu bakar swiddiq akiwakumbusha kwa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
“Hakuwa Muhammad , rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani, ni kiumbe aina nyingine, isipokuwa yeye ni Mtume wa jinsi ya Mitume wengine waliokuweko kabla yake, anafikisha ujumbe wa Mola wake. Basi iwapo atakufa, kwa kumalizika muda wake, au atauawa, kama walivyoeneza uvumi maadui, kwani mtarudi nyuma na kuacha dini yenu na kuyaacha aliyowaletea Mtume wenu? Basi yeyote miongoni mwenu atakayerudi nyuma akaiacha dini yake, yeye hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote, bali ataidhuru nafsi yake madhara makubwa. Ama atakayekuwa na msimamo imara juu ya Imani yake na akamshukuru Mola wake juu ya neema ya Uislamu, hakika Mwenyezi Mungu Atamlipa malipo mazuri kabisa”.
[Al-Imran: 144].
Basi aliposikia Omar aya hizi hakuvumilia isipokuwa alianguka na akazimia.
Huyu ndiye Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu, na mwisho wa manabii na mitume alimtuma Mwenyezi Mungu kwa watu wote akiwapa bishara njema na kuwaonya na akafikisha ujumbe na akatekeleza amana na akaupa umma nasaha .
Alimpa nguvu Mwenyezi Mungu kwa Qur’ani tukufu iliyoteremshwa kutoka mbinguni, Qur’ani ambayo
“Batili haikifikii kutoka upande wowote katika pande Zake, na hakuna kitu chenye kuibatilisha, kwani hiyo imetunzwa isipunguzwe wala isizidishwe. Ni uteremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya waja Wake, Mwenye kushukuriwa kwa sifa za ukamilifu Alizonazo”.
[Surat Fuswilat 42]
Qur’ani ambayo kama wangekusanyika wanadamu kuanzia wa mwanzo ilipoumbwa dunia mpaka wa mwisho ili wapate kuleta mfano wake, hawataweza kuleta mfano wake hata kama wao kwa wao wangekuwa ni wenyekusaidiana.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“Enyi watu Muabuduni Mwenyezi Mungu Ambaye kakuumbeni nyinyi na Akawaumba waliokuwa kabla yenu, ili muwe ni miongoni mwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu”.
Mola wenu ni Yule Aliyewafanyia ardhi iwe ni tandiko, ili maisha yenu yawe mepesi juu yake, na mbingu ziwe zimejengeka madhubuti, na Akateremsha mvua kutoka mawinguni, Akatoa kwa mvua hiyo matunda na mimea aina mbali mbali ili iwe ni riziki kwenu. Basi, msimuwekee Mwenyezi Mungu washirika katika ibada, hali nyinyi mnajua kuwa Mwenyezi Mungu Amepwekeka katika kuumba, kuruzuku na kustahiki kuabudiwa.
Na mkiwa, enyi makafiri, mna shaka juu ya Qurani tuliyomteremshia mja wetu Muhammad, Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani, na mkadai kuwa haitoki kwa Mwenyezi Mungu, basi leteni sura moja inayofanana na sura ya Qurani, na takeni msaada kutoka kwa yeyote mnayemuweza ili awasaidie, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.
Mkiwa hamuwezi sasa, na hamtaweza wakati unaokuja kabisa, basi uogopeni Moto, kwa kumuamini Nabii, Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani, na kumtii Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa kwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake.
Waambie, ewe Mtume, watu wa Imani na amali nzuri, habari yenye kuwajaza furaha, kuwa wao huko Akhera watakuwa na Mabustani ya ajabu, ambayo inapita mito chini ya majumba yake makubwa na miti yake yenye vivuli. Kila Anapowaruzuku Mwenyezi Mungu humo aina yoyote ya matunda yenye ladha, watasema, “Mwenyezi Mungu Alituruzuku aina hii ya matunda kipindi cha nyuma.” Watakapoionja wataikuta ladha yake ni tofauti na ladha yake (yaani: na ile ladha ya duniani), ingawa inafanana na aina iliyopita kwa rangi, sura na jina. Na katika hayo Mabustani ya Peponi watakuwa na wake waliosafishika na kila aina ya uchafu, wa nje, kama mkojo na damu ya hedhi, na wandani, kama kusema uongo na kuwa na tabia mbaya. Na wao, katika Pepo na starehe zake, watakaa milele, hawafi humo wala hawatoki”.
[Al Baqara: 21-25].
Na hii Qur’ani imejengeka kwa sura mia moja na kumi na Nne (114), ndani yake kuna aya elfu sita, Mwenyezi Mungu anawapa changamoto wanadamu kwa zama zote zilizopita kuwa walete sura moja tu mfano wa hii Qur’ani, na sura fupi zaidi katika Qur’ani zimejengeka kwa aya tatu tu.
Basi ikiwa wataweza kufanya hivyo (kuleta mfano wa Qur’ani) basi nawajue kuwa hii Qur’ani haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Na huu ni muujiza mkubwa ambao Mwenyezi Mungu amempa msaada Mtume wake -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- kama alivyo mpa msaada Mwenyezi Mungu kwa miujiza mingine isiyo ya kawaida, miongoni mwayo:
E- Kupewa Msaada Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- kwa miujiza mbali mbali:
1- Alikuwa anamuomba Mwenyezi Mungu na anaweka mkono wake katika chombo yanatibuka maji kutoka katika vidole vyake na wanakunywa wanajeshi maji hayo, idadi yao ni zaidi ya elfu moja .
2- Na alikuwa akimuomba Mola wake na anaweka mkono wake katika chakula na chakula kinaongezeka katika sahani mpaka kinatosha kuliwa na maswahaba Elfu moja na mia tano.
3- Na alikuwa akiinua mikono yake mbinguni akimuomba Mwenyezi Mungu kuteremsha mvua, basi alikuwa haondoki sehemu ile aliyoombea mpaka yabubujike maji kutoka usoni kwake Mtukufu kutokana na athari ya mvua na miujiza mingine mingi.
Na akampa Mwenyezi Mungu msaada wa kumuhifadhi na wala hawezi yeyote kumfikia kwa yule atakaye kumuuwa na atakaye kuificha nuru ambayo amekuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu.
“Ewe Mtume, fikisha wahyi wa Mwenyezi Mungu uliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako. Na iwapo utapunguza bidii katika kuufikisha, ukaficha chochote katika wahyi huo, basi utakuwa hukuufikisha ujumbe wa Mola wako. Na kwa hakika, Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alifikisha ujumbe wa Mola wake kikamilifu. Basi yeyote atakayedai kuwa yeye alificha chochote, katika yale aliyoteremshiwa, atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake uongo mkubwa. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwenye kukulinda na kukuokoa na maadui zako. Si juu yako lolote isipokuwa ni kufikisha. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hamuelekezi kwenye uongofu aliyepotea njia ya haki na akayapinga uliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu”.
[Al Maaida: 67].
Hakika alikuwa Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- pamoja na kupewa msaada na Mwenyezi Mungu -ni kiigizo chema katika matendo yake yote na kauli zake,na alikuwa wa mwanzo kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu zinazoteremka juu yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na alikuwa ni miongoni mwa wenye pupa ya kufanya ibada na utiifu, na ni mkarimu, hakibakii kitu mikononi mwake katika mali isipokuwa ataitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa kuwapa maskini na mafukara na wenye kuhitaji, bali hata urithi aliwaambia maswahaba wake kuwa:
“Sisi jopo la Manabii haturithiwi, chochote tulichokiacha ni sadaka”
[2] Hadithi hii ameitoa imamu Ahmad (2/463) na sanadi yake ni sahihi kama alivyotaja ahmad shaakir katika kuhakiki musnad (19/92Hawasigaiwe warithi wangu hata dinari moja chochote nilichokiwacha baada ya kutoa matumizi ya wake zangu na malipo ya mfanyakazi ni sadaka )
Ama kuhusu tabia zake hakuna awezaye kuzifikia, hakuandamana na yeyote isipokuwa alimpenda toka ndani ya moyo wake, hivyo basi anakuwa Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- ndiye kipenzi mkubwa kwake yeye kuliko watoto wake na mzazi wake na watu wote.
Anasema Anas bin Maalik mtumishi wa bwana Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- “sikuwahi kugusa kiganja kizuri na kilaini wala chenye kunukia zaidi kuliko kiganja cha Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kwa hakika nilimuhudumia miaka kumi na wala hakuwahi kuniambia kwa kitu nilichokifanya kwanini umekifanya, wala sijawahi kuacha kufanya kitu akaniambia kwanini hukufanya “[3].
[3] Ameitoa hadithi hii Imamu Bukhariy (4/230)
Huyo ndiye Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye Mwenyezi Mungu ameiinua heshima yake na akuinua utajo wake kwa walimwengu wote, na wala hatajwi mwanadamu katika huu ulimwengu leo hii na kabla ya leo kama anavyotajwa yeye, tangu mwaka Elfu moja na mia Nne, mamilioni ya vipaza sauti katika pande zote za ulimwengu vinamtangaza kila siku mara tano kwa kusema: “Nashuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu ” mamilioni ya wenye kusali wanarudia rudia kila siku mara kumi kwa kusema “Nashuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu”.
F- Maswahaba watukufu :
Waliibeba Maswahaba watukufu Da’wa ya uislamu baada ya kufa kwa bwana Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na wakaenda nayo mashariki mwa ardhi na magharibi yake, na walikuwa kiukweli ni walinganiaji bora wa dini hii, na walikuwa kwa hakika ni watu wakweli katika kuongea kwao na wenye uadilifu mkubwa na wingi wa kutunza Amana, na wenye pupa ya kuwaongoa watu na kuwaenezea kheri.
Walijipamba na sifa za mitume na wakawaiga kwa sifa zao, na ikawa kwa tabia hizi athari yake ni ya wazi katika kukubalika kwa dini hii kwa mataifa ya duniani, watu wakaingia mfululizo katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kutoka Afrika magharibi mpaka mashariki ya Asia na mpaka katikati mwa bara la ulaya kwa kuuipenda dini hii bila kulazimwishwa wala kutenzwa nguvu.
Hakika hao ni Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ambao ni watu bora baada ya manabii, na walio Maarufu kati yao ni makhalifa wanne ambao walihukumu dola ya kiislamu baada ya kufa kwa bwana Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na wao ni :
1- Abubakari Swidiiq.
2- Omar bin khattwab.
3- Othman bin Affaan.
4- Ally bin Abii Twaalib.
Waislamu wanawatambua maswahaba hawa kwa kina na wanawaheshimu, na wanajikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kumpenda Mtume wake na kuwapenda Maswahaba wa Mtume wake wote, wake kwa waume na wanawatukuza na wanawaheshimu na kuwaweka katika nafasi zao wanazostahiki.
Wala hakuna mwenye kuwachukia na kuwavunjia heshima yao isipokuwa yule mwenye kuikufuru dini ya uislamu hata kama atadai kuwa yeye ni muislamu, Mwenyezi Mungu amewasifia kwa kauli yake.
{Mmekuwa Umma bora mlioteuliwa kwa ajili ya watu mnaamrisha mema na mnakataza mabaya na mnamuamini Mwenyezi Mungu}
[Al-Imran: 110]
Na alithibitisha Radhi zake kwao pale walipompa Mtume -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- kiapo cha utiifu Akasema: Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“Mwenyezi Mungu Ameridhika na Waumini pale walipokupa mkono wa ahadi, ewe Mtume, chini ya mti (Hii ndio hiyo Bay ‘ah al-Ridwān ya hapo Ḥudaybiyah). Mwenyezi Mungu Alijua yaliyomo ndani ya nyoyo za Waumini hawa ya Imani, ukweli na utekelezaji ahadi, basi Mwenyezi Mungu Akawateremshia utulivu, Akaziimarisha nyoyo zao na Akawapa, badala ya kile kilichowapita katika mapatano ya Ḥudaybiyah, ufunguzi wa karibu, nao ni ufunguzi wa kuiteka Khaybar.
(Suratil fat-hi 18)