Nguzo za Imani.
Na ikifahamika kuwa nguzo za uislamu kuwa ni alama za wazi ambazo anazitekeleza muislamu na kuwa utekelezaji wake unajulisha juu ya kushikamana na uislamu wake, basi kuna nguzo zingine ndani ya moyo ambazo inapasa kwa muislamu kuziamini ili uislamu wake uwe sahihi, na nguzo hizo huitwa nguzo za imani, kila kinapozidi kiwango chake katika moyo wake ndivyo anavyozidi kupanda daraja la imani na anastahiki kuingia katika waja wa Mwenyezi Mungu walioamini, na daraja hili ni daraja kubwa sana kwa waislamu, kwani kila Muumini ni muislamu lakini si kila muislamu ni muumini ambaye kaifikia daraja ya waumini.
Ni jambo la hakika kuwa ana asili ya imani lakini yawezekana asiwe na imani iliyokamilika.
Na nguzo za Imani ni sita
Ni kumuamini Mwenyezi Mungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume wake na siku ya mwisho na kuamini Qadari kheri yake na shari yake.
Basi nguzo ya kwanza: Ni kumwamini Mwenyezi Mungu, na kunaujaza moyo kumpenda Mwenyezi Mungu na kumtukuza na kujidhalilisha kwake na kuonyesha unyonge mbele yake na kutii maamrisho yake yeye peke yake hana mshirika wake, kama unavyoujaza moyo hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu, na kutarajia yaliyoko kwake, ili mtu awe ni katika waja wa Mwenyezi Mungu wachamungu na wenye kufuata njia iliyonyooka.
Nguzo ya pili: Ni kuwaamini Malaika na kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu wameumbwa kwa nuru na idadi yao hakuna aijuaye kutokana na wingi wao mbinguni na ardhini isipokuwa Mwenyezi Mungu, wameletwa kwa ajili ya ibada na kumtaja Mwenyezi Mungu na kumtakasa ,”Wanamtakasa usiku na mchana wala hawachoki”,
“Hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa yale aliyowaamrisha na wanafanya yale walioamrishwa”
{Surat Tahriim 6}
Na kila mmoja wao anakazi yake ambayo Mwenyezi Mungu amemfanyia wepesi, miongoni mwao kuna wenye kuibeba Ar-shi (Napo ni mahali alipotulizana Mwenyezi Mungu),na wengine wamewakilishwa kutoa roho, na wengine huteremka na wahyi kutoka mbinguni naye ni Jibrili -juu yake amani- na ndiye mbora wao, na wengine ni walinzi wa peponi na kuna walinzi wa motoni na wengine wasiokuwa hao katika Malaika wema wanao wapenda waumini wa kibinadamu, na wanazidisha kuwatakia msamaha kwa Mwenyezi Mungu na kuwaaombea dua.
Nguzo ya Tatu; Kuviamini vitabu vilivyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Basi Muislamu huamini kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha vitabu kwa amtakaye katika Mitume wake vitabu ambavyo vimekusanya kheri na ukweli na mambo ya uadilifu kutoka kwake Mtukufu, na akateremsha kwa nabii Mussa Taurati na kwa Issa Injili na kwa Daudi Zaburi na kwa Ibrahim Swahifa, na hivi vitabu havizingatiwi uwepo wake kama alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama anavyoamini kuwa Mwenyezi Mungu ameiteremsha Qur’ani kwa Mtume wa mwisho wa Mitume naye ni Muhammad -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani- na kuwa yeye ameteremsha Aya kwa utaratibu wa kufuatana kwa muda wote wa miaka ishirini na tatu na akazihifadhi Mwenyezi Mungu zisibadilishwe wala kugeuzwa.
“Hakika sisi tumeiteremsha Qur’ani kwa Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukie, na hakika sisi tunachukua ahadi kuitunza isiongezwe, isipunguzwe wala sehemu yoyote katika hiyo isipotee”.
[A Hijri: 9].
Nguzo ya Nne : Kuwaamini Mitume.
Na yametangulia maneno kuhusu hao mitume kwa ufafanuzi zaidi na kuwa umma zote zilizotangulia katika Historia nzima hakika aliwatumia mitume na dini yao ni moja, na Mola wao ni mmoja na wanawalingania wanadamu kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu yeye na wakiwatahadharisha kutokana na ukafiri na ushirikina na maasi.
“Na hakuna umma wowote uliopita isipokuwa alipita kwao muonyaji”
{Surat Faatir 24}
Nao hao Mitume ni wanadamu kama wanadamu wengine aliwachagua Mwenyezi Mungu ili kufikisha ujumbe wake:
{Hakika sisi tumekuletea wahyi, ewe Mtume, ili ufikishe ujumbe kama tulivyomletea wahyi Nuhu na Manabii wengine baada yake. Na tumewapelekea wahyi Ibrāhīm, Ismā’īl, Is-ḥāq, Ya‘qūb na Kizazi chake, nao ni Manabii waliokuwa katika makabila kumi na mbili ya wana wa Isrāeli wanaotokana na kizazi cha Ya’qūb, na pia ‘Īsā, Ayyūb, Yūnus, Hārūn na Sulaimān na tukampa Dāwūd Zaburi, nacho ni kitabu na kurasa zilizoandikwa}.
Na tumewatuma Mitume ambao tumekuelezea habari zao katika Qur’ani, kabla ya aya hii, na Mitume wengine ambao hatukukuelezea habari zao kwa hekima tuliyoikusudia. Na Mwenyezi Mungu Alisema na Mūsā waziwazi ili kumtukuza kwa sifa hii. Katika aya hii tukufu kuna uthibitisho wa sifa ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ya kusema kama inavyolingana na utukufu Wake, na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Alisema na Nabii Wake Mūsā, amani imshukie, kikweli bila ya mtu wa kati (baina yao).
Nimewatuma wajumbe kwa viumbe wangu wakatoe habari njema ya malipo yangu mema na waonye juu ya adhabu yangu, ili wanadamu wasiwe na hoja watakayoifanya ni kisingizio cha udhuru baada ya kuwatuma Mitume. Na daima Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika mamlaka Yake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji wake wa mambo”.
{An-nissa 163-165}
Muislamu anawaamini hao Mitume wote na anawapenda wote na anawanusuru wote, na wala hawatofautishi kati yao, na mwenye kumkufuru yeyote kati ya hao Mitume au akamtukana na akamuudhi kwa hakika anakuwa amewakufuru wote.
Na mbora wao na mtukufu wao kwa cheo mbele ya Mwenyezi Mungu ni Mwisho wa Manabii ambaye ni Muhammad -Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani.
Nguzo ya Tano: Kuamini siku ya mwisho.
Na kuwa Mwenyezi Mungu atawafufua waja kutoka kwenye makaburi yao na atawafufua siku ya kiyama wote ili awahesabu kutokana na matendo yao ya maisha ya hapa duniani.
“Na malipizo ya Mwenyezi Mungu ya kuwatesa maadui Wake Siku ya Kiyama yatakuwa kwenye siku ambayo itabadilishwa ardhi hii kwa ardhi nyingine nyeupe iliyotakata kama fedha, na vile vile zitabadilishwa mbingu kwa nyingine, na watatoka viumbe makaburini mwao wakiwa hai wakiwa wamejitokeza kukutana na Mwenyezi Mungu Aliye Mmoja, Mwenye kutenza nguvu, Aliyepwekeka kwa utukufu Wake, majina Yake, sifa Zake na matendo Yake na kulazimisha Kwake kila kitu”.
{Surat Ibrahiim 48}
“Pindi mbingu zitakapopasuka na ukaharibika mpango wake.
Na pindi nyota zitakapoangukiana.
Na pindi Mwenyezi Mungu Atakapozifanya bahari kulipuka na maji yake kutoweka.
Na pindi makaburi yatakapogeuzwa kwa kufufuliwa waliomo ndani yake.
Wakati huo itajua kila nafsi na vitendo vyake vyote ilivyovifanya, vilivyotangulia na vilivyoahirika na italipwa kwa vitendo hivyo”.
{Suratul infitaar 1-5}
“Kwani haoni mwanadamu anayekanusha kufufuliwa vile umbo lake lilivyoanza akapata kuchukua dalili ya kuwa atarudishwa kuwa hai, kwamba sisi tumemuumba kwa tone la manii lililopitia hatua tofauti mpaka akawa mkubwa, na ghafla anageuka kuwa ni mwingi wa utesi aliyejitolea wazi kwa kujadiliana?
Na mkanushaji Kufufuliwa alitupigia mfano usiofaa kupigwa, nao ni kulinganisha uweza wa Muumba na ule wa muumbwa, na akasahau kulianzaje kule kuumbwa kwake. Alisema, «Ni nani mwenye kuhuisha mifupa iliyochakaa na kumumunyuka?
Mwambie, «Atakaye ihuisha ni Yule Aliyeiumba mara ya kwanza, na Yeye kwa viumbe vyake vyote ni Mjuzi, hakifichikani Kwake yeye kitu chochote.
«Ambaye Amewatolea, kwenye mti wa kijani ulio mbichi, moto unaochoma, ambao kwa mti huo mnawasha moto.» Yeye Ndiye Anayeweza kutoa, kwenye kitu, kinyume chake. Katika hayo pana dalili ya upweke wa Mwenyezi Mungu na ukamilifu wa uweza Wake, na miongoni mwa uweza huo ni kuwatoa wafu kutoka makaburini mwao wakiwa hai.
Je, kwani hakuwa yule aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni Mwenye uweza wa kuumba mfano wao, Akawarudisha kama Alivyowaanzisha? Ndio, kwa kweli Yeye Analiweza hilo. Na Yeye ni Mwenye sifa kamilifu za uumbaji viumbe vyote , Aliye Mjuzi wa kila Alichokiumba na Atakachokiumba, hakuna kinachofichikana kwake.
Hakika amri Yake Anapotaka kitu kiwe ni kukiambia, «Kuwa!» Na kikawa. Na kati ya hizo ni kufisha, kuhuisha, kufufua na kukusanya.
Ameepukana Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kutakasika, na uelemevu na kuwa na mshirika. Yeye Ndiye Mwenye kumiliki kila kitu, Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake bila ya kuwa na mshindani au mpinzani. Na zimejitokeza dalili za uweza Wake na ukamilifu wa neema Zake. Na Kwake Yeye mtarejea ili muhesabiwe na mlipwe.”
{Surat Yasiin 73-77}
“Na Mwenyezi Mungu Ataiweka Mizani ya uadilifu kwa ajili ya Hesabu katika siku ya Kiyama. Hawatodhulumiwa hawa wala wengine kitu chochote, hata kama ni kitendo, kizuri au kibaya, cha kadiri ya mdudu chungu mdogo, kitazingatiwa katika hesabu ya mwenyewe. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyadhibiti matendo ya waja Wake na ni Mwenye kuwalipa kwayo”.
[Al Anbiyaai: 47].
{Basi anaye tenda chembe ndogo ya wema, atauona! Na anaye tenda chembe ndogo ya uovu atauona!} ((278)).
[Azzalzalat: 7-8].
Na hufunguliwa milango ya moto kwa yule anayestahiki ghadhabu za Mwenyezi Mungu na hasira zake na adhabu zake zenye kuumiza, na hufunguliwa milango ya pepo kwa waumini ambao wanatenda yaliyo mema.
{Na watawapokea Malaika na kuwaambia hii ndiyo siku yenu ambayo mlikuwa mkiahidiwa}
{suratil An-biyaai 103}
“Na waongozwe wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake kuelekezwa upande wa Jahanamu makundi kwa makundi, na watakapoifikia itafunguliwa milango yake saba na wale washika hazina wake waliowakilishwa kuisimamia hiyo Jahanamu. Na hao washika hazina watawakaripia kwa kusema, «Vipi nyinyi mlimuasi Mwenyezi Mungu na mkakataa kuwa Yeye ni Mola wa haki Peke Yake.? Kwani hamkutumiwa Mitume miongoni mwenu wanaowasomea aya za Mola wenu na kuwaonya na misukosuko ya Siku ya Leo?» Watasema wakikubali makosa yao, «Ndio, walitujia na ukweli Mitume wa Mola wetu na wakatuonya na Siku ya Leo, lakini lishathibiti neno la Mwenyezi Mungu kwamba adhabu Yake itawafikia wenye kumkanusha Yeye.»
Na wataongozwa wale waliomcha Mola wao, kwa kumpwekesha na kufanya vitendo vya utiifu Kwake, wapelekwe Peponi, makundi kwa makundi. Na watakapoifikia na waombewe kuingia, milango yake itafunguliwa, na Malaika waliowakilishwa kuisimamia Pepo watawakongowea (watawapongeza) na watawaamkia kwa ucheshi na furaha kwa kuwa wamesafishika na athari za maasia na watawaambia, «Amani iwe juu yenu! Mmesalimika na kila baya. Hali zenu ni nzuri. Basi ingieni Peponi mkae milele humo.»
Na hapo Waumini watasema, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetuhakikishia ukweli wa ahadi Yake Aliyotuahidi kupitia kwa ndimi za Mitume Wake, na Akaturithisha ardhi ya Pepo tukawa tunashukia kwenye ardhi hiyo popote pale tunapotaka. Ni mazuri yaliyoje malipo ya watu wema waliojitahidi kumtii Mola wao.»
{Surat Zumar 71-75}
Hii ndiyo pepo ambayo ndani yake kuna Neema ambazo jicho halijawahi kuona wala sikio halikuwahi kusikia wala moyo wa mwanadamu haukuwahi kufikiria.
“Hakuna nafsi yoyote inayoyajua yale aliyowawekea Mwenyezi Mungu hawa Waumini ya kutuliza macho na kufurahisha moyo, yakiwa ni malipo yao kwa matendo yao mema.
Je, Yule Aliyekuwa mtiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, mwenye kuamini agizo lake la kuwalipa mema wema wenye kufanya mema na kuwalipa ubaya wenye kufanya mabaya, ni kama yule aliyemkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume wake na akaikanusha Siku ya Kiyama? Hawalingani mbele ya Mwenyezi Mungu.
Ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na wakayafanya yale waliyoamrishwa kwayo, basi malipo yao ni mabustani ya Pepo watashukia huko na watakaa kwenye starehe zake wakiandaliwa, yakiwa malipo yao kwa yale waliokuwa wakiyafanya ulimwenguni ya utiifu Kwake.
Na ama wale waliotoka nje ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu na wakafanya matendo ya kumuasi, basi mahali pao pa kutulia ni moto wa Jahanamu, kila wakitaka kutoka wanarudishwa ndani. Na wataambiwa, kwa kulaumiwa na kukaripiwa, «Onjeni adhabu ya Moto ambayo mlikuwa mkiikanusha ulimwenguni.»
{Surat Sajidah 17-20}
“Sifa ya Pepo ambayo Mwenyezi Mungu Amewaahidi wachamungu: ndani yake kuna mito mikubwa ya maji yasiyobadilika, na mito ya maziwa yasiyogeuka utamu wake, na mito ya shizi (pombe) ambayo wanaionea ladha wenye kuinywa, na mito ya asali iliyosafishwa isiyo na taka. Na wachamungu hawa watapata ndani ya hiyo pepo matunda yote ya aina tofauti na mengineyo. Na kubwa kuliko hayo ni kule kusitiriwa na kusamehewa dhambi zao. Basi je, wale watakaokuwa ndani ya Pepo hiyo ni kama wale watakaokaa Motoni bila kutoka humo na wakanyweshwa maji yaliyo moto sana hadi ya mwisho yakawakata tumbo zao?”
{Surat Muhammad 15}
“Hakika wachamungu watakuwa kwenye mabustani ya Pepo na neema kubwa.
Watajistarehesha kwa vile Alivyowapa Mwenyezi Mungu vya neema miongoni mwa aina mbalimbali za ladha na starehe, na Atawaokoa Mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya Moto.
Kuleni chakula kwa furaha, na mnywe kinywaji chenye ladha, yakiwa ni malipo ya matendo mema mliyoyafanya duniani
Nao watakuwa wameegemea, wako juu ya vitanda vinavyoelekeana, na tutawaoza wanawake weupe wenye macho mapana yaliyo mazuri.
(Surat Tuur 17- 20)
Atujaalie Mwenyezi Mungu tuwe ni katika watu wa peponi.
Nguzo ya sita: Kuamini Qadar kheri zake na shari zake.
Na kuwa kila harakati hapa ulimwenguni ni makadirio yaliyoandikwa toka kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka jambo lake
“Hampatwi na msiba wowote, enyi watu, kwenye ardhi wala ndani ya nafsi zenu, utokanao na magonjwa, njaa na ndwele (maradhi), isipokuwa umeandikwa kwenye Ubao Uliyohifadhiwa kabla ya kuumbwa viumbe. Hakika hilo, kwa Mwenyezi Mungu, ni jambo sahali (jepesi)”.
Suratil Hadid 22
“Hakika sisi kila kitu tumekiumba kwa kipimo tulichokikadiria na kukipitisha, na ilitangulia elimu yetu ya kukijua kitu hicho na kukiandika kwenye Ubao Uliohifadhiwa”.
(Al- qamar 49)
“Je, hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu anavijua vilivyomo mbinguni na ardhini ujuzi kamili Aliouthibitisha katika Ubao Uliohifadhiwa? Ujuzi huo ni jambo sahali kwa Mwenyezi Mungu Ambaye hakuna kitu kinachomshinda”.
Al-hajj 70
Hizi nguzo sita atakaye zikamilisha na akaziamini kiukweli anakuwa ni katika waja wa Mwenyezi Mungu walioamini, na viumbe wote wanatofautiana katika daraja za imani wanazidiana baadhi yao wao kwa wao, na daraja la juu kabisa la imani ni daraja la Ihsan (wema) nalo nikufikia katika nafasi ya “Kumuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamuona na kama haumuoni basi yeye anakuona” [5]
Na hawa ndiyo viumbe bora watakaofaulu kwa kupata Daraja la juu peponi katika makazi ya Firdausi.
[5] ametoa hadithi hii Al-bukhaariy4777