Dini ya Uislamu

Inatangazwa kupitia Dalili zitokanazo na Qur'ani na Sunnah za Mbora wa Viumbe.

Neno la Tauhidi (Laa ilaaha illa llaahu) Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Msingi muhimu wa dini ya kiislamu ni neno la Tauhidi (Laa ilaaha illa llahu) na bila msingi huu madhubuti jengo la uislamu haliwezi kusimama imara, na hilo ni neno la kwanza ambalo anatakiwa kulitamka mtu mwanzo anapoingia katika uislamu akiwa analiamini neno hilo na kuamini maana zake zote na vyenye kutokana na maana yake. Basi ni nini maana ya (Laa ilaaha illa llahu)?

Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu makusudio yake ni:

– Hakuna muumba wa Ulimwengu isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee.

– Hakuna Mmiliki na muendeshaji wa huu Ulimwengu isipokuwa ni Mwenyezi Mungu pekee.

-Hakuna Mwenye kuabudiwa anayestahiki kufanyiwa ibada isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee.

Mwenyezi Mungu ndiye aliyeuumba ulimwengu huu mpana na mzuri wa hali ya juu. Mbingu hizi na nyota zake kubwa na Sayari zake zenye kutembea, zinatembea katika nidhamu iliyopangika vyema, na harakati za kupendeza, hakuna mwenye kuzishika mbingu hizo isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na Ardhi hii na milima yake na mabonde yake na mito yake, na miti yake na mimea yake, pamoja na hewa yake na maji yake, nchi kavu yake na bahari yake, na kila mwenye kuishi humo na mwenye kutembea juu yake, bila shaka kabisa vyote hivi ameviumba Mwenyezi Mungu na akavileta kutoka katika kutokuwepo.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’ani tukufu:

“Na alama kwao (ya utendaji kazi wa Mwenyezi Mungu) ni jua ambalo linatembea hadi kituo chake Alichokikadiria Mwenyezi Mungu, halitakipita kituo hicho wala halitatulia kabla ya kukifikia. Huo ni mpango wa Mshindi Asiyeshindwa, Mjuzi Ambaye hakuna kitu chochote kinachofichikana katika ujuzi Wake”.

“Na mwezi ni alama katika viumbe vyake. Tumeukadiria uwe na njia za kupitia kila usiku. Unaanza ukiwa mwezi mwandamo mdogo sana na unaendelea kuwa mkubwa mpaka unakuwa mwezi mkamilifu mviringo, kisha unarudi kuwa mdogo kama shuke la mtende kuuku lililolegea”.

“Kila kimojawapo kati ya jua, mwezi, usiku na mchana, kina wakati ambao Mwenyezi Mungu Ameukadiria, na hakitangulii kikapita wakati huo. Haiwezekani kwa jua kuufikia mwezi likaufuta mwangaza wake au ukageuza njia yake ya kupitia. Na haiwezekani kwa usiku kuutangulia mchana ukauingilia kabla ya wakati wake kumalizika. Na kila kimojawapo kati ya jua, mwezi na nyota viko katika anga vinaogelea”.

[Surat Yaasin 38- 40].

“Na ardhi tumeipanua na kuitandika, na tukaweka humo majabali yaliyojikita, ili ardhi isiende mrama na watu wake, na tukaotesha humo kila aina ya mimea yenye mandhari ya kupendeza na yenye kunufaisha, inayomfurahisha mwenye kuiangalia”.

“Ili viwe ni mazingatio ya kumfanya mtu aone na atoke kwenye giza la ujinga, na ni ukumbusho kwa kila mja mnyenyekevu, mwenye kucha (kumcha Mungu) na kuogopa, mwenye kurejea sana kwa Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na kutukuka”.

“Na tumeteremsha kutoka juu mvua yenye manufaa mengi, tukaotesha kwayo mabustani yenye miti mingi na nafaka za mimea ya nafaka zinazovunwa”.

“Na tukaotesha mitende mirefu yenye makarara yaliyojaza na kupandana”.

[Surat Qaaf 7-10]

Huu ndiyo uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, Ameifanya Ardhi kuwa ni tulivu na akaweka humo vyenye kuvutia kwa kiwango kinachoendana na uhitaji wa maisha, Basi hazidishi mpaka ikawa ni uzito kutembea juu yake, wala hapunguzi kiasi cha kushindwa kuenea humo viumbe hai na kila kitu kwake yeye kimewekwa kwa kiasi maalumu.

na ameshusha kutoka mawinguni maji yaliyo masafi na wala hayawezi kuendelea maisha isipokuwa kupitia maji.

{Na tumejaalia kutokana na maji kila kitu kuwa Hai}

[Al Anbiyaai 30].

Na akatoa kutokana na maji mimea na matunda na wakanyweshelezwa kwa maji hayo wanyama na wanaadamu, na akaiandaa ardhi ili iyahifadhi maji hayo na akafuatishia humo chemchem na mito.

Na akaotesha katika ardhi mabustani yenye kuvutia kwa miti na maua yake na uzuri wake wenye kuvutia Mwenyezi Mungu Ambaye ameumba kila kitu kwa namna nzuri na akaanza kumuumba mwanadamu kutokana na udongo.

Hakika mwanadamu wa kwanza aliyemuumba Mwenyezi Mungu ni Baba wa wanadamu naye ni Adam – juu yake amani- kisha akamtengeneza sawa na akamuwekea sura na akampulizia roho itokayo kwake , kisha akamuumba kutokana na huo udongo mke wake kisha, akakifanya kizazi chake kilichotokana na udongo kikatokana na maji madhalilifu (Manii).

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Na kwa hakika tulimuumba Ādam kutokana na udongo uliochukuliwa kutoka ardhi yote”.

“Kisha tukamuumba kwa tone la manii”

“Kisha tukaliumba tone hilo kwa kuligeuza kulifanya pande la damu iliyo nyekundu, kisha tukaliumba pande la damu kwa kuligeuza kulifanya kinofu cha nyama kadiri ya kutafunika baada ya siku arobaini, na tukakiumba kinofu cha nyama kilicho laini kwa kukigeuza kukifanya mifupa, na tukaivisha nyama ile mifupa, kisha tukamfanya ni kiumbe kingine kwa kupulizia roho ndani yake. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mwenye kheri nyingi Ambaye Ametengeneza umbo la kila kitu”.

[Al Mu’uminun: 12-14].

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Mnayaonaje maji ya manii mnayoyatupa ndani ya vizazi vya wake zenu”,

“Je nyinyi ndio mnaomuumba mwanadamu kutokana na hayo au ni sisi ndio wenye kuumba?”

“Sisi tumekadiria kati yenu kifo na wala hatutoshindwa kuwafufueni” tena.

“Na sisi si wenye kushindwa kubadilisha umbo lenu Siku ya Kiyama na kuwaumba kwa sifa na namna msizozijua”.

[Suratil Waaqiyah 58-68].

Zingatia kukuumba kwako Mwenyezi Mungu utaona maajabu makubwa kutokana na kuweka vyombo vidogo sana na nidhamu iliyo na mpangilio maalumu ambao haijulikani kazi yake isipokuwa twajua kidogo sana licha ya kujua mpangilio wake, kwa mfano hiki chombo kilichokamilika kwa ajili ya kumeng’enya chakula, mpangilio wake unaanzia kwenye mdomo kwa kukata chakula vipande vidogo ili iwe ni wepesi katika kusaga na kisha hatua ya kooni hutupa tonge kwenye koromeo na hufungua mlango wa kudaka tonge na kufunga mlango wa hewa kisha tonge huteleza kwenda tumboni kwa kupitia kidaka tonge chenye kutikisika mtikisiko kama mdudu,

Na kwenye utumbo mpana kunaendelea kazi ya kumenge’nya chakula na hapo kinabadilika chakula na kuwa kimiminika kinachofungua tundu la utumbo mpana na kuelekea kwenye maingilio ya utumbo mwembamba na huko hundelea kazi ya kumeng’enya ambayo ni kazi ya kukibadilisha chakula kutoka kwenye hali yake ya uchakula (ghafi) na kukifanya kufaa kuwa lishe ya viungo vya mwili.

Kisha kutoka katika utumbo mpana chakula huelekea kwenye utumbo mwembamba na hapo ndipo hukamilika umenge’nyaji wa mwisho na kwa sura hii chakula kinakuwa ni chenye kufaa kunyonywa kupitia nyuzinyuzi zilizopo kwenye Matumbo ili kipite pamoja na mfumo wa damu.

Na hicho ni chombo kilichokamilika cha mzunguko wa damu ambao huzunguka katika mishipa ya damu iliyofungana na lau kama itanyooshwa urefu wake ungezidi zaidi kilomita elfu moja zilizoshikana katika pampu iliyopo katikati huitwa moyo. Moyo huo hauchoki katika kuhamisha damu kupitia mishipa hiyo imara.

Na kuna chombo kingine cha kupumulia, na cha Nne ni cha neva-Mishipa- na cha Tano ni cha kutoa uchafu, na cha Sita na Saba na mpaka cha Kumi ni katika vile ambavyo tunaendelea kuvijua kila siku na vile tusivyovijua ni vingi kuliko tunavyovijua. Basi ni nani aliyemuumba huyu mwanadam kwa namna hii nzuri asiyekuwa Mwenyezi Mungu?.

Kwa hivyo ni kosa kubwa sana hapa ulimwenguni kumfanyia Mwenyezi Mungu mshirika hali ya kuwa yeye ndiye aliyekuumba wewe.

Elekea kwa moyo mkunjufu na kwa roho safi na zingatia mwanzo wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu hewa ambayo unayoivuta na inapenya kuja kwako toka katika sehemu pasi na kuonekana rangi yake, na lau kama ingekatika hewa hiyo kwa dakika chache ungekosekana uhai, Hakika haya maji ambayo unayoyanywa, na hicho chakula ambacho unakila, na mwanadamu umpendaye, na hii Ardhi ambayo unatembea juu yake, na ile mbingu ambayo unaiona, kila ambacho macho yako yanakiona na yasichokiona katika viumbe vikubwa au vidogo, vyote hivyo ni viumbe vya Mwenyezi Mungu Muumba aliye mjuzi wa mambo yote.

Hakika kufikiria viumbe vya Mwenyezi Mungu vinatujuza utukufu wa Mwenyezi Mungu na uwezo wake, na miongoni mwa watu wapumbavu wa hali ya juu na wajinga na waliopotea ni mwenye kuona huu uumbaji uanzilishi mtukufu ulioshikana uliopangika, wenye kujulisha juu hekima ya hali ya juu na uwezo usiokuwa na mipaka, kisha mtu huyo hamuamini muumba ambaye amemfanya awepo kutoka katika kutokuwepo. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Je, wameumbwa hawa washirikina bila kuwepo mwenye kuwaumba na kuwapatisha au wao wamejiumba wenyewe?” Na yote mambo mawili haya yametenguka na hayawezekani. Na kwa hivyo, inalazimika kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba, na Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye hakuna anayepasa kuabudiwa, wala kufaa kuabudiwa, isipokuwa Yeye.

“Au wao wameumba mbingu na ardhi kwa ustadi huu wa kipekee? Bali wao hawaamini adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wao ni washirikina”.

[Attur: 35-36].

Hakika Mwenyezi Mungu kutakasika na machafu ni kwakwe na mtukufu, linamtambulisha uwepo wake umbile salama pasina kuwa na haja ya kufundishwa, hakika amelifanya umbile ni lenye kujikuta katika kuumbwa kwake ni lenye kuelekea na kukimbilia kwake, lakini umbile hilo ni lenye kupotoshwa na kuwekwa mbali naye – Mwenyezi Mungu aliyetakasika na machafu.

Na hivyo ikiwa atapatwa na tatizo, msiba au dhiki ya hali ya juu na matatizo na yakampata majanga makubwa akiwa pwani au baharini, atakimbilia moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu kutaka kutoka kwake msaada na kuepushwa na aliyokuwa nayo, na Mwenyezi Mungu- kutakasika na machafu ni kwake- humjibu aliyedhurika pindi anapomuomba na humuondoshea mabaya.

Na huyu Muumba mtukufu ni mkubwa kuliko kila kitu, hapimishwi na chochote katika viumbe wake, naye ni mkubwa ambaye ukubwa wake hauna ukomo wala hakuna mwenye ujuzi uliokamilika kwa kujua hilo. Mwenye kusifika na sifa za utukufu wa hali ya juu zaidi ya viumbe wake juu ya mbingu zake.

“Hapana kitu mfano wake, naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona”

[Ash-shura: 11].

Hafanani na chochote katika viumbe vyake na lolote ulifikirialo akilini mwako kuhusu yeye basi Mwenyezi Mungu hayuko hivyo.

Anatuona Mwenyezi Mungu akiwa juu ya mbingu zake na sisi hatumuoni:

“Macho hayamuoni Mwenyezi Mungu ulimwenguni. Ama kwenye nyumba ya Akhera, Waumini watamuona Mola wao bila kumueneza. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, anayafikia macho na kuyazunguka, na kuyajua vile yalivyo. Na Yeye ni Al-Latīf (Mpole) kwa mawalii Wake (vipenzi vyake), Anayejua mambo yenye upeo wa udogo, Al-Khabīr (Mtambuzi) Anayejua mambo ya ndani”.

[Suratul An’aam 103],

Bali hisia zetu na nguvu hazistahamili kumuona hapa duniani.

Na kwa hakika mmoja miongoni mwa Manabii wa Mwenyezi Mungu alitaka kumuona, naye ni Nabii Mussa -Amani iwe juu yake- na Mwenyezi Mungu alipomsemesha mbele ya mlima Sinai: Akasema Ewe Mola wangu jitokeze ili nikuone, akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kumwambia Mussa:

«Hutoniona!»Yaani hutaweza kuniona ulimwenguni. «Lakini liangalie jabali, likitulia mahali lilipo ndipo nitakapojitokezea, basi utaniona.» Alipojitokeza Mola wake kwa lile jabali alilifanya lipondeke liwe sawa na ardhi. Hapo Mūsā alianguka akazimia. Alipopata fahamu kutoka kwenye hali ya kuzimia alisema, «Umetakasika, ewe Mola wangu, na kila sifa isiyolingana na utukufu wako, mimi natubia kwako kutokana na kuomba kwangu kukuona katika uhai huu wa kiulimwengu, na mimi ni wa mwanzo wa wenye kukuamini miongoni mwa watu wangu.»

[Suratul Aaraf 143],

Basi ule mlima mkubwa na mrefu ulisambaratika na kusagikasagika kwa kutokeza kwake Mwenyezi Mungu, basi vipi anaweza mwanadamu kuhimili kwa nguvu zake zilizo dhaifu na mnyonge.

Na katika sifa za Mwenyezi Mungu – kutakasika na machafu ni kwake – ni kuwa kwake yeye juu ya kila kitu ni muweza.

{Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kushindwa na chochote kilichopo mbinguni wala Ardhini}

[surat faatwir 44].

Mkononi mwake kuna uhai na kifo. Wanahitajia kutoka kwake viumbe wote, naye ni mwenye kujitosheleza kwa viumbe vyote Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Enyi watu! Nyinyi ndio wahitaji kwa Mwenyezi Mungu katika kila kitu, hamjitoshelezi Naye hata kiasi cha kupepesa jicho. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Mwenye kujitosheleza na watu na kila kitu miongoni mwa viumbe Vyake, Mwenye kushukuriwa kwa dhati Yake na majina Yake na sifa Zake”, Anayeshukuriwa kwa neema Zake. Kwani kila neema waliyo nayo watu inatoka Kwake. Sifa njema zote ni Zake na shukrani kwa kila namna.

[Surat Faatwir 15].

Na miongoni mwa sifa zake – kutakasika na machafu ni kwake – Ni ujuzi wake ulioenea katika kila kitu:

“Na kwa Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka na kuwa juu, kuna( mafātih al-ghayb), yaani: Funguo za hazina za mambo ya ghaibu yaliyofichikana, hakuna azijuwazo ila Yeye. Miongoni mwazo ni ujuzi wa Kiyama, kuteremka mvua, viliyomo ndani ya zao, matendo ya siku zinazokuja na mahala mtu atakapokufa. Na Anajua kila kilichoko barani na baharini. Na hakuna jani, linaloanguka kutoka kwenye mmea wowote, isipokuwa Analijua. Na kila chembe iliyofichikana ardhini na kila kibichi na kikavu, kimethibitishwa kwenye kitabu kilicho wazi kisicho na utatizi nacho ni Al-Lawh(Al-Maḥfūẓ ( Ubao Uliohifadhiwa)

[Al An’am: 59].

Anajua yote yanayozungumzwa na ndimi zetu na yanayo fanywa na viungo vyetu bali yanayofichwa na vifua vyetu yote hayo anayajua.

“Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Anakijua kile kinachopitishwa na mtazamo wa macho kwa njia ya siri na kuiba na kile ambacho mtu anakidhamiria katika nafsi yake kizuri au kibaya”.

[Surat Ghaafir 19].

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kutufuatilia na mwenye kujua hali zetu hakijifichi kwake yeye chochote kilichopo Ardhini wala mbinguni haghafiliki wala hasahau wala halali, Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye hakuna yeyote anayestahiki uungu na kuabudiwa isipokuwa Yeye. Ndiye Aliye hai Ambaye Amekusanya maana yote ya uhai mkamilifu unaolingana na utukufu Wake. Ndiye Msimamizi wa kila kitu. Kusinzia hakumshiki wala kulala. Kila kilichoko mbinguni na kilichoko ardhini ni miliki Yake. Na hatojipa ujasiri mtu yeyote kuombea mbele Yake isipokuwa kwa ruhusa Yake. Ujuzi Wake umevizunguka vitu vyote vilivyopita, vilivyoko na vitakavyo kuja. Anajua yaliyo mbele ya viumbe katika mambo ambayo yatakuja na yaliyo nyuma yao katika mambo yaliyopita. Na hakuna yeyote, katika viumbe, mwenye kuchungulia chochote katika elimu Yake isipokuwa kadiri ile ambayo Mwenyezi Mungu Amemjulisha na kumuonyesha. Kursiy Yake imeenea kwenye mbingu na ardhi. Kursiy ni mahali pa nyayo za Mola, uliyo mkubwa utukufu Wake, na hakuna ajuwaye namna ilivyo isipokuwa ni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Wala hakumuelemei Mwenyezi Mungu Aliyetakata kuzitunza. (hizo mbingu na ardhi).Yeye Ndiye Aliye juu ya viumbe Vyake vyote, kwa dhati Yake na sifa Zake, Aliyekusanya sifa za utukufu na kiburi”. Aya hii ni aya tukufu zaidi katika Qur’ani, na inaitwa Āyah al- Kursīy.

[Al Baqara: 255].

Ana sifa zilizokamilika ambazo hazina mapungufu wala aibu.

Ana majina mazuri na sifa za hali ya juu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ana Majina Mazuri yanayoonyesha ukamilifu wa uwezo Wake, na majina Yake yote ni mazuri. Basi ombeni kutoka Kwake, kwa majina Yake, mnachotaka na waacheni wale wanaogeuza majina Yake kwa kuzidisha na kupunguza au kupotoa, kama kumuita kwa majina hayo asiyeyastahiki, kama vile washirikina wanavyowaita, kwa majina hayo, waungu wao, au ayape majina hayo maana ambayo Mwenyezi Mungu Hakuitaka wala Mtume Wake. Basi watapata malipo ya matendo yao mabaya waliokuwa wakiyafanya ulimwenguni ya kumkanusha Mwenyezi Mungu, kuyapotoa majina Yake na kuwafanya waongo Mitume Wake”.

[Suratul Al-aaraf 180].

Na Mwenyezi Mungu -kutakasika na machafu ni kwake- hana mshirika wake katika ufalme wake wala hana msaidizi wala wa kufananishwa naye.

Ametakasika -kutakasika na machafu ni kwake- kuwa na mke na pia kuwa na mtoto, bali yeye amejitosheleza kwa hayo yote Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Sema, ewe Mtume, «Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyepwekeka kwa ustahiki wa kuabudiwa, uumbaji na utakatifu wa Majina na Sifa, Asiye na mshirika katika hayo”.

«Mwenyezi Mungu Ambaye Peke Yake Ndiye Mwenye kukusudiwa kwa kukidhi haja na matakwa.

«Hakuzaa wala hakuzaliwa.

«Wala hakuna yeyote katika viumbe Vyake mwenye kufanana wala kushabihiyana naye katika Majina Yake, Sifa Zake wala vitendo Vyake.»

[Al Ikhlaswi: 1-4].

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Na hawa makafiri walisema, «Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto.»

“Kwa hakika mmeleta, enyi wenye wasemaji, kwa kusema neno hili, jambo kubwa lililo baya.

“Zinakaribia mbingu kupasuka kwa ubaya mkubwa wa neno hilo, ardhi kuvunjika vipande-vipande majabali kuanguka kwa nguvu kwa kukasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu”

“kwa kumnasibishia mtoto, Mwenyezi Mungu”.

“Haifai kwa Mwenyezi Mungu na hainasibiani na Yeye Awe na mtoto, kwani kuwa na mtoto ni dalili ya upungufu na mahitajio, na Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi Mwenye kuhimidiwa Aliyeepukana na sifa zote za upungufu”.

“Hakuna aliye mbinguni, miongoni mwa Malaika, wala aliye ardhini, miongoni mwa binadamu na majini, isipokuwa atamjia Mola wake Siku ya Kiyama akiwa ni mja mdhalilifu mnyenyekevu mwenye kukubali uja wake Kwake”.

[Mariam: 88-93].

Na yeye -aliyetakasika na machafu-ni mwenye kusifika na sifa za utakasifu na uzuri na nguvu na utukufu na utawala na ufalme na nguvu.

Na yeye vile vile husifika na sifa ya ukarimu na msamaha na huruma na hisani, hivyo yeye ni mwingi wa rehema ambayo imeenea rehema yake kila kitu.

Mwenye kurehemu ambaye huruma yake imeishinda hasira zake.

Na ni mkarimu ambaye ukarimu wake hauna ukomo wala hazina yake ya ukarimu haiishi.

Na majina yake yote ni mazuri yanajulisha juu ya sifa zilizokamilika ambazo hapasi kua na sifa hizo isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Na kuzijua sifa zake kunauzidishia moyo mapenzi na utukufu, na kuogopa na kunyenyekea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Na kwa hivyo basi inakuwa maana ya Laa ilaaha illa llaahu ni kuwa kisifanywe chochote ambacho ni katika ibada isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na hakuna mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kusifika na sifa za Uungu na ukamilifu naye ndiye muumba mwenye kutoa riziki mwenye kuneemesha mwenye kuhuisha mwenye kufisha, aliye bora zaidi kwa viumbe wake basi yeye pekee ndiye anayestahiki kuabudiwa na hana mshirika wake.

Na yeyote atakaye kataa ibada ya Mwenyezi Mungu au akamuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kwa hakika atakuwa ameshirikisha na amekufuru.

Na haipasi kusujudu na kurukuu na kunyenyekea na kusali isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Na wala haombwi msaada isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala haelekewi kwa dua isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala usiombe haja yoyote isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na wala hakutafutwi ukaribu kwa namna yeyote wala utiifu wa kuabudiwa isipokuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Sema,«Hakika Swala yangu na kuchinja kwangu wanyama, na uzima wangu na kufa kwangu yote ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu muumba wa walimwengu wote.

«Asiye na mshirika katika uungu Wake wala katika Ulezi Wake wala katika majina Yake na sifa Zake. Kumpwekesha huko Mwenyezi Mungu kulikosafishika ndiko Alikoniamrisha mimi Mola wangu, Aliyetukuka na kuwa juu. Na mimi ni wa kwanza kumfuata Mwenyezi Mungu kikamilifu katika umma huu.»

[Suratul An-am 162-163].

About The Author

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *