Kwanini Ametuumba Mwenyezi Mungu?
Majibu ya swali hili zito yako katika umuhimu wa hali ya juu lakini ni lazima kutegemea majibu kutoka katika wahyi wa Mwenyezi Mungu, Basi Mwenyezi Mungu ndiye ambaye ametuumba na yeye ndiye ambaye anatupa habari kuhusu lengo lake la kutuumba sisi, amesema – aliyetukuka jambo lake-
“Na sikuumba majini na binadamu na kutimiliza Mitume wote isipokuwa kwa lengo tukufu, nalo niabudiwe mimi Peke Yangu, na sio asiyekuwa mimi”.
[Adh Dhariyati: 56].
Hivyo Utumwa, ndiyo sifa inayowakusanya viumbe wote wa Mwenyezi Mungu viumbe ambao hakuna awezaye kuidhibiti idadi yake, miongoni mwao ni Malaika na wengineo, ni katika maajabu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu, umma wote huu una umbile uliloumbiwa kwa kujengewa maisha ya kuwa ni wenye kumuabudu na kumtakasa Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote.
“Zinamtakasa Yeye, kutakata ni Kwake, mbingu saba na ardhi na viumbe wote waliyo humo. Na kila kitu kilichoko katika ulimwengu huu kinamuepusha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na sifa za upungufu, maepusho yanayofungamana na kumsifu na kumshukuru, kutakata ni Kwake, lakini nyinyi, enyi watu, hamtambui hilo. Kwa kweli, Yeye ni Mpole kwa waja Wake, hawaharakishii adhabu wanaomuasi, ni Mwingi wa msamaha kwao”.
[Al- israa 44].
Na Malaika wanausiwa na kulazimishwa kujitakasa kama ambavyo wanadamu wanausiwa kuzitakasa nafsi.
Lakini Utumwa wa mja kumuabudu Mola wake ni wa hiyari na siyo wa kulazimishwa (Ni hiyari na hiyari hiyo ni mtihani)
“Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafanya nyinyi mpatikane kutoka kwenye hali ya kutokuwepo, kati yenu kuna wenye kuukanusha uungu Wake na baadhi yenu kuna wenye kuuamini na kufuata Sheria Zake kivitendo. Na Yeye, kutakasika na kila sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwenye kuviona vitendo vyenu, hakuna chochote chenye kufichikana Kwake, na Atawalipa kwavyo”.
[Surat Taghaabun 2]
“Je hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, wanamsujudia Yeye, katika hali ya kunyenyekea na kufuata amri, Malaika walioko mbinguni, viumbe walioko ardhini, jua, mwezi, majabali, miti na wanyama? Na wanamsujudia Mwenyezi Mungu, kwa kutii na kwa hiari, watu wengi, nao ni Waumini. Na kuna watu wengi imepasa adhabu juu yao, na kwa hivyo wao ni watwevu (madhalili). Na yeyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemtweza (Amemdhalilisha) hakuna yeyote wa kumtukuza. Hakika Mwenyezi Mungu Anafanya kwa viumbe vyake Atakalo kulingana na hekima Yake”.
[Suratil Hajj 18]
Mwenyezi Mungu ametuumba ili tumuabudu na atupime ufaulu wetu katika kufanikisha ibada hii, Basi yeyote atakaye muabudu Mwenyezi Mungu na akampenda na akanyenyekea kwake na akatii maamrisho yake na akajiepusha na makatazo yake, Hupata radhi za Mwenyezi Mungu na rehema zake na mapenzi yake na Mwenyezi Mungu humlipa malipo yaliyo mazuri.
Na atakaye kataa kumuabudu Mwenyezi Mungu ambaye amemuumba na akamruzuku, na akafanya kiburi kwa kuacha kufanya ibada, na akakataa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na makatazo yake, basi huyo atakuwa anastahiki Hasira za Mwenyezi Mungu na machukizo yake na adhabu yake iumizayo, na Mwenyezi Mungu Mtukufu hakutuumba bure bure na wala hakutuacha hivi hivi, na hakika mtu mjinga zaidi na mpumbavu kuliko watu wote ni mwenye kudhani kuwa yeye amekuja humu duniani na akapewa usikivu na uoni na akili, kisha akaishi katika maisha haya muda fulani kisha akafa, na wala hajui kwanini amekuja humu ulimwenguni na ni wapi atakwenda baada ya kufa, na Mwenyezi Mungu aliyetakasika na mtukufu anasema:
“Je, mlidhania, enyi viumbe, ya kwamba sisi tuliwaumba nyinyi mkiwa mumepuuzwa: hakuna maamrisho wala makatazo wala malipo mema wala mateso, na kwamba nyinyi hamtorudishwa kwetu Akhera kwa Hesabu na Malipo?”
[Al Mu’uminun: 115].
Na wala hafanani kwa Mwenyezi Mungu mwenye kumuamini yeye na akategemea kwake na akataka kuhukumiwa kwa sheria zake, na akawa anampenda anayenyenyekea kwake na anajikurubisha kwake kwa kufanya ibada mbalimbali na kutafuta yenye kumridhisha kila mahala, mtu mwenye kufanya hayo hafanani na mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu ambaye amemuumba na akamwekea sura na anazipinga alama zake na dini yake na anakataa kufuata maamrisho yake.
Huyu mtu wa kwanza anapata Ukarimu na Thawabu na mapenzi na Radhi, na huyu mwingine anapata kuchukiwa na adhabu.
pale ambapo Mwenyezi Mungu atawafufua watu baada ya kufa kwao kutoka makaburini mwao na akamlipa mwema wao neema mbalimbali na kumkirimu katika pepo yenye neema na kuadhibiwa mkosaji mwenye kiburi aliyekataa kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumuadhibu katika nyumba ya adhabu.
Na ni wajibu juu yako kufikiria ukubwa wa takrima anayopewa mwema pindi zinapokuwa hizi thawabu na takrima kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliye jitosheleza na mkarimu ambaye hana ukomo katika takrima zake na rehema zake na wala haiishi hazina yake. Hakika thawabu hizi zitakuwa na thamani kubwa peponi haziishi wala haziondoki (Na habari hizi ndizo tutakazozizungumzia hivi punde),
Na vile vile unatakiwa kufikiria adhabu kali na yenye kuumiza kwa kafiri, wakati itakapotoka adhabu toka kwa Mwenyezi Mungu mwenye nguvu ambaye hakuna ukomo wa nguvu zake.