Dini ya Uislamu

Inatangazwa kupitia Dalili zitokanazo na Qur'ani na Sunnah za Mbora wa Viumbe.

K- Mtume Mussa -Amani iwe juu yake.

Kisha akazuka katika mji wa Misri mfalme muovu mwenye kiburi, anaitwa Fir’auni anadai uungu na kuwa wamuabudu yeye na anawachinja awatakao na kuwadhulumu awatakao,akatupa habari Mwenyezi Mungu kuhusu Firauni kwa maneno yake:

“Hakika Fir’awn alifanya kiburi na akapita mipaka katika nchi, akawafanya watu wake kuwa ni makundi tofauti-tofauti, akawa analinyongesha kundi moja ya hayo, nalo ni lile la Wana wa Isrāīl, akawa anawaua watoto wao wa kiume na anawabakisha wanawake wao kwa kutumika na kudharauliwa, Hakika yeye alikuwa ni miongoni mwa waharibifu katika ardhi.

“Na tunataka kuwafadhili wale ambao Fir’awn aliwafanya wanyonge nchini, tuwafanye ni viongozi katika wema na ni wenye kuulingania, na tuwafanye wao wairithi nchi baada ya kuangamia Fir’awn na watu wake”.

Na tuwape uthabiti katika nchi na tumfanye Fir’awn, Hāmān na askari wao waone, kutoka kundi hili linalonyongeshwa kile walichokuwa wakikiogopa cha kuangamia kwao na kuondoka ufalme wao na kuwatoa wao kwenye nyumba zao kwa mkono wa mzaliwa wa Wana wa Isrāīl.

“Na tukampa mawazo mama yake Mūsā alipomzaa na akamuogopea asije Fir’awn akamchinja kama anavyowachinja watoto wa wana wa Isrāeli kwamba «mnyonyeshe ukiwa mtulivu, na pindi uogopapo kujulikana mambo yake, muweke sandukuni na ulitupe kwenye mto wa Nail bila ya kuogopa kwamba fir’awn na watu wake watamuua na bila ya kuwa na masikitiko ya kuwa mbalinaye, hakika sisi tutamrudisha kwako na tutamtumiliza kuwa Mtume.»

Hapo akamuweka sandukuni na akalitupa kwenye mto Nail, na wafuasi wa Fir’awn wakalipata na wakalichukua, na mwisho wake ukawa vile Alivyokadiria Mwenyezi Mungu kuwa Mūsā awe ni adui yao kwa kuwa kinyume na dini yao, na awatie kwenye huzuni ya kuzamishwa na kuondokewa na ufalme wao mikononi mwake. Kwa hakika, Fir’awn na Hāmān na wasaidizi wao walikuwa wafanyaji makosa washirikina.

Na mke wa Fir’awn alipomuona , Mwenyezi Mungu Alimtia mapenzi moyoni mwake na akasema kumwambia Fir’awn, «Mtoto huyu atakuwa chimbuko la furaha kwangu mimi na wewe, Msimuue kwani huenda tukapata kheri kutoka kwake au tumfanye ni mtoto wetu» na hali Fir’awn na jamaa wa nyumbani kwake hawafahamu kwamba maangamivu yao yatatokea mikononi mwake.

Na kifua cha mama yake Mūsā kikawa hakijishughulishi na kitu chochote duniani isipokuwa hamu ya Mūsā na kumtaja, na alikaribia kudhihirisha kuwa yule ni mwanawe lau si sisi kumthibitisha, naye akavumilia asilidhihirishe hilo, ili awe ni miongoni mwa wenye kuamini ahadi ya Mwenyezi Mungu na mwenye kuwa na yakini nayo.

Na akasema mama yake Mūsā kumwambia nduguye wa kike alipomtupa mtoni, «Fuata athari za Mūsā uone atafanywa nini? Akafuata athari zake na akamuona kwa mbali na hali watu wa Fir’awn hawajui kwamba yeye ni dada yake na kwamba yeye anafuatilia habari zake.

Na tulimzuia Mūsā asinyonye kutoka kwa wanyonyeshaji kabla hatujamrudisha kwa mama yake, hapo dada yake akasema, «Je, ni waonyeshe watu wa nyumba ambao watamlea na kumnyonyesha vizuri na ambao watakuwa na huruma naye? Wakamkubalia hilo.

Basi tukamrudisha Mūsā kwa mama yake, ili jicho lake litulie kwake na tukamtekelezea ahadi yetu kwake, kwa kuwa alirudi kwake akiwa amesalimika na kuuawa na Fir’awn, na ili asihuzunike kwa kuepukana naye, na ajue kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, ile Aliyowaahidi kuwa atawarudishia na Amfanye ni miongoni mwa Mitume. Hakika Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake, lakini wengi wa washirikina hawajui kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli.

Na Alipofikia Mūsā umri wa kuwa na nguvu na ikakamilika akili yake, tulimpa busara na elimu ya kutambua hukumu za Sheria. Na kama tulivyompa Mūsā malipo mema kwa utiifu wake na wema wake, tunampa malipo mema mwenye kufanya wema miongoni mwa waja wetu.

Na Mūsā aliingia mjini kwa kujificha wakati ambapo watu wake walikuwa wako katika hali ya kughafilika, akawapata humo watu wawili wanapigana, mmoja wao ni katika wana wa Isrāeli jamaa za Mūsā na mwingine ni katika jamaa za Fir’awn. Basi yule aliyekuwa ni katika jamaa ya Mūsā alitaka msaada dhidi ya yule Aliyekuwa katika maadui zake, hapo Mūsā akampiga ngumi na akafa. Mūsā akasema alipomuua, «Huu ni katika ushawishi wa Shetani aliyenipandisha hasira zangu mpaka nikampiga huyu akafa. Hakika ya Shetani ni adui wa mwanadamu ni mwenye kupoteza njia ya uongofu, ni mwenye uadui wa waziwazi.» Kitendo hiki cha Mūsā kilikuwa kabla ya kupewa unabii.

Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu kwa kumuua mtu ambaye hukuniamuru kumuua, basi nisamehe dhambi hilo.» Na Mwenyezi Mungu Akamsamehe. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe sana dhambi za waja Wake, ni Mwenye huruma nao sana.

Mūsā akasema, «Mola wangu! Kwa vile ulivyonineemesha kwa toba, msamaha na neema nyingi, sitakuwa mwenye kumsaidia yeyote kufanya uasi wake na uhalifu wake.

Hivyo basi Mūsā akaingiwa na khofu akiwa kwenye mji wa Fir’awn, anatafuta habari zinazozungumzwa na watu kuhusu yeye na yule mtu aliyemuua, hapo akamuona yule mtu wake wa jana akipigana na Mmisri mwingine na akimtaka amsaidie. Mūsā alimwambia, «Kwa kweli, wewe ni mwingi wa upotofu, ni mpotevu waziwazi.»

Basi alipotaka Mūsā kumshika Mmisri kupambana naye, alisema, «Je, unataka kuniua mimi kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki isipokuwa kuwa jeuri katika nchi, na hutaki kuwa ni miongoni mwa wale wanaofanya upatanishi kati ya watu.»

Na akaja mtu mmoja mbiombio kutoka mwisho wa mji, akasema, «Ewe Mūsā! Kwa hakika wale watukufu wa jamii ya Fir’awn wanafanya njama ya kukuua na wanashauriana juu ya hilo, basi toka. Kwani mimi ni kati ya wale wanaokupa ushauri mzuri na wanaokupendelea wema.»

Hapo Mūsā akautoka mji wa Fir’awn akiwa katika hali ya kuogopa, akitazamia kukamatwa na wale wanaomtafuta, na akamuomba Mwenyezi Mungu Amuokoe na watu madhalimu.

Na alipokusudia kuelekea nchi ya Madyan, na akatoka nje ya utawala wa Fir’awn, alisema, «Nina matumaini kwamba Mola wangu Ataniongoza njia nzuri ya kuelekea Madyan.»

Alipoyafikia maji ya Madyan, alilikuta hapo kundi la watu wanawapa maji wanyama wao, na akawakuta, kando ya kundi hilo, wanawake wawili wamejitenga na watu na wamewazuilia wanyama wao na pale penye maji, kwa kushindwa kwao na udhaifu wao wa kutoweza kubanana na wanaume, na wanangojea mpaka wanyama wa watu waondoke kwenye maji kisha hapo wawapatie wanyama wao maji. Mūsā, amani imshukie, alipowaona aliwaonea huruma, kisha alisema kuwaambia, «Mna nini nyinyi?» wakasema, «Hatuwezi kubanana na wanaume, na hatuchoti maji mpaka watu wamalize kuchota, na baba yetu ni mzee sana hawezi kuwachotea maji wanyama wake kwa udhaifu wake na uzee wake.»

Basi Mūsā akawachotea maji wanyama wa wale wanawake wawili, kisha akageuka kwenda kwenye kivuli cha mti kujifunika nacho na akasema, «Mola wangu! Hakika mimi ni muhitaji wa wema wako wowote ule utakaoniletea,» kama vile chakula. Na njaa ilikuwa imemshika sana.

Hapo akaja mmoja wa wale wanawake wawili aliowachotea maji akitembea na huku akiona haya akasema, «Baba yangu anakuita ili akupe malipo ya maji uliyotuchotea.» Na Mūsā akaenda naye hadi kwa baba yake. Alipomjia baba yake na akamsimulia habari zake yeye pamoja na Fir’awn na watu wake, yule baba wa mwanamke alisema, «Usiogope! Umeokoka na watu madhalimu, nao ni Fir’awn na watu wake, kwani wao hawana mamlaka yoyote nchini kwetu.»

Akasema mmoja wa wanawake wawili kumwambia baba yake, «Ewe baba yangu! Muajiri yeye akuchungie wanyama wako, kwani mtu bora wa wewe kumuajiri kwa kuchunga ni yule aliye na nguvu ya kuwalinda wanyama wako, aliye muaminifu ambaye huchelei kuwa atakufanyia hiana katika amana unayompatia.»

Mzee akasema kumwambia Mūsā, «Mimi nataka kukuoza mmoja wa mabinti wangu hawa wawili, kwa sharti uwe muajiriwa wangu wa kuwachunga wanyama wangu kwa kipindi cha miaka minane. Na ukikamilisha miaka kumi, basi hiyo ni hisani yako. Na mimi sitaki kukusumbua kwa kuifanya miaka kumi. Utanikuta mimi, Mwenyezi Mungu Akitaka, ni miongoni mwa watu wema, katika uzuri wa tangamano na utekelezaji wa ahadi ya ninayoyasema.

Mūsā akasema, «Hilo ulilolisema lisimame kuwa ndio ahadi baina yangu mimi na wewe, muda wowote wa vipindi viwili nitakaa kazini, nitakuwa nimekutekelezea, na sitatakiwa kuongeza juu yake, na Mwenyezi Mungu, kwa tunayoyasema, ni Mtegemewa, ni Mtunzi, Anatuona na Anakijua kile tulichofanya mapatano juu yake.»

Basi Nabii wa Mwenyezi Mungu Mūsā, amani imshukie, alipomtekelezea mwenzake kipindi cha miaka kumi, nao ni muda mkamilifu zaidi wa vile vipindi viwili, na akaenda na watu wa nyumbani kwake kuelekea Misri, aliona moto upande wa jabali la Ṭūr. Mūsā alisema kuwaambia watu wa nyumbani kwake, «Subirini na mngojee. Mimi nimeona moto. Huenda nikawaletea habari kutoka kule, au nikawaletea kijinga cha moto mkapata kuota nacho.»

Basi Mūsā alipoujia moto, Mwenyezi Mungu Alimuita kutoka upande wa bonde la mkono wa kulia wa Mūsā, katika ardhi iliyobarikiwa ya upande wa mti kwamba: «Ewe Mūsā! Mimi Ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote,»

na kwamba: «itupe fimbo yako!» Na Mūsā akaitupa, ikageuka kuwa nyoka anayetembea kwa haraka. Alipoiona inatetemeka kana kwamba ni nyoka kama walivyo nyoka wengine, aligeuka kumkimbia na hakugeuka kwa kuogopa. Na hapo Mola wake Alimuita, «Ewe Mūsā! Nielekee mimi, na usiogope! Wewe ni miongoni mwa wenye kuaminika na kila lenye kuchukiza.

«Tia mkono wako kwenye mfuko wa kanzu yako uliofunguliwa kifuani na uutoe, utatoka ukiwa mweupe, kama barafu, weupe ambao si wa ugonjwa wala mbalanga, na ujikumbatie kwa mikono yako ili usalimike na hofu. Hivi viwili nilivyokuonyesha, ewe Mūsā, vya fimbo kugeuka nyoka na kuufanya mkono wako kuwa mweupe na wenye kung’ara, si kwa ugonjwa wala mbalanga, ni dalili mbili kutoka kwa Mola wako, uende nazo kwa Fir’awn na watukufu wa watu wake.» Hakika Fir’awn na viongozi walio karibu naye walikuwa ni wakanushaji.

Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi nimemuua mtu wa jamii ya Fir’awn, basi naogopa wasije wakaniua.

Na ndugu yangu, Hārūn, ana ufasaha zaidi wa matamshi kuliko mimi, basi mtume yeye pamoja na mimi awe msaidizi wangu, ataniamini na atawafafanulia wao yale ninayowaambia. Mimi ninachelea wasije wakanikanusha mimi kwa maneno yangu nitakayowaambia kwamba mimi nimetimilizwa kwao.»

Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Tutakupa nguvu kwa ndugu yako, na tutawapa nyinyi wawili hoja juu ya Fir’awn na watu wake wasiweze kuwafikia nyinyi kwa ubaya wowote. Nyinyi wawili na wale wenye kuwaamini nyinyi ndio mtakaopewa ushindi juu ya Fir’awn na watu wake kwa sababu ya aya (miujiza) yetu na ukweli unaoonyeshwa na aya hizo.»

[Suratul Qaswasi 4-35]

[1] Mama yake alimuweka katika sanduku, na akamtupa nalo katika mto Nile.

Basi akaondoka na ndugu yake Haruna kwenda kwa -Mfalme Mwenye kiburi- wakimlingania katika kumuabudu Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote.

Fir’awn akamwambia Mūsā, «Na huyo Mola wa viumbe wote Ambaye unadai kwamba wewe ni mjumbe Wake, ni kitu gani?»

Mūsā akasema, «Yeye ni Mmiliki na Mwenye kuiendesha mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya viwili hivyo. Iwapo nyinyi mna yakini na hilo, basi aminini.»

Fir’awn akasema kuwaambia walioko pembezoni mwake miongoni mwa watukufu wa watu wake, «Je, hamsikii maneno ya Mūsā ya ajabu kwamba kuna mola asiyekuwa mimi?»

Mūsā akasema, «Mola Ambaye mimi nawalingania nyinyi Kwake ni Yule Aliyewaumba nyinyi na Aliyewaumba wa mwanzo. Basi vipi nyinyi mnamuabudu ambaye ni kiumbe kama nyinyi na yeye ana mababa waliotoweka kama mababa zenu?»

Fir’awn akasema kuwaambia wale watu wake makhsusi akiwapandisha ghadhabu zao, kwa kuwa Mūsā amemkanusha yeye, «Kwa kweli, huyu mjumbe wenu aliyeletwa kwenu ni mwendawazimu , anasema maneno yasiyofahamika.»

Mūsā akasema, «Mola wa Mashariki na Magharibi na vilivyoko baina ya viwili hivyo, na vilivyomo ndani yake vya mwangaza na giza. Hili linapelekea kuwa ni lazima kumuamini Yeye Peke Yake, iwapo nyinyi ni miongoni mwa watu wa akili na kuzingatia.»

Fir’awn akamwambia Mūsā kwa kumtisha, «Ukichukua mwingine asiyekuwa mimi ukamfanya ni mola nitakufunga jela pamoja na wale niliowafunga.»

Mūsā akasema, «Je, utanifanya mimi ni miongoni mwa wafungwa jela, hata nikikuletea hoja ya kukata ambayo kwa hoja hiyo utabainika ukweli wangu?»

Fir’awn akasema, «Basi ilete ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli katika madai yako.»

Hapo Mūsā aliitupa fimbo yake na ikageuka nyoka mkubwa anayeonekana waziwazi.

Na akauvuta mkono wake kutoka kwenye uwazi wa kanzu iliyofunguliwa kifuani au chini ya kwapa lake, na papo hapo ukawa mweupe kama maziwa usio na mbalanga, ukiwa ni alama kwa Fir’awn; akiurejesha unarudi rangi yake ya mwanzo, kama ulivyo mwili wake.

Fir’awn akasema kuwaambia watukufu wa watu wake, kwa kuogopa wasije wakaamini, «Kwa kweli Mūsā ni mchawi hodari.

Anataka kuwatoa nyinyi, kwa uchawi wake, kwenye ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani kuhusu yeye nipate kuyafuata maoni yenu?»

Watu wake wakamwambia, «Msubirishe Mūsā na Hārūn, na utume askari mijini wawakusanye wachawi.

Watakujia na kila anayejua uchawi na akawa hodari kuufahamu.»

Wakakusanywa wachawi, na wakapangiwa wakati maalumu, nao ni wakati wa mchana wa siku ya Pambo ambayo wanajitenga na shughuli zao, na wanajikusanya na kujipamba, ili wakutane na Mūsā

na wawahimize watu kujumuika kwa matarajio kwamba ushindi uwe ni wa wachawi.

Sisi tunatarajia ushindi uwe ni wa wachawi ili tujikite kwenye dini yetu.

Na wachawi walipomjia Fir’awn walimwambia, ‘Je, sisi tutakuwa na malipo ya mali au heshima ikiwa tutakuwa ni wenye kumshinda Mūsā?»

Fir’awn akasema, «Ndio, nyinyi mtapata kwangu malipo mnayoyataka, na nyinyi hapo mtakuwa ni miongoni mwa wenye kusogezwa karibu na mimi.»

Mūsā akasema kuwaambia wachawi, akitaka kuutangua uchawi wao na kuonyesha kuwa kile alichokileta si uchawi, «Tupeni mtakavyovitupa vya uchawi.»

Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na zikawadhihirikia watu kwenye akili zao kuwa ni nyoka wanaotembea, na wakaapa kwa enzi ya Fir’awn kwa kusema, «Sisi ni wenye kushinda.»

Hapo akaitupa Mūsā fimbo yake, na papo hapo ikawa ni nyoka mkubwa, akawa anavimeza vile vilivyotokana na wao, hao wachawi, vya uzushi wa bandia.

Waliposhuhudia hilo na wakajua kuwa halitokani na udanganyifu wa wachawi, walimuamini Mwenyezi Mungu na wakamsujudia.

Wakasema, «Tumemuamini Mola wa viumbe wote.

«Naye ni Mola wa Mūsā na Hārūn.» Naye ni yule Ambaye lazima ibada ielekezwe Kwake, Peke Yake, si kwa mwingine.

Fir’awn akasema kuwaambia wachawi kwa kukataa, «Mmemkubali Mūsā bila ya idhini yangu!» Na akasema akiashiria kuwa kitendo cha Mūsā ni uchawi, «Yeye ni mkubwa wenu aliyewafundisha nyinyi uchawi, basi mtayajua mateso yatakayowafikia. Nitaikata mikono yenu na miguu yenu kwa kuitawanya: kwa kuukata mkono wa kulia na mguu wa kushoto au kinyume chake, na nitawasulubu nyote.»

Wachawi walisema kumwambia Fir’awn, «Hakuna madhara ya duniani yatakayotupata, kwa kweli sisi ni wenye kurudi kwa Mola wetu, Atupe neema ya kuendelea.

Sisi tunataraji Mola wetu Atusamehe makosa yetu ya ushirikina na mengineyo kwa kuwa sisi ndio Waumini wa mwanzo katika watu wako.»

Na Mwenyezi Mungu Akampelekea wahyi Mūsā, amani imshukie, kwamba, «Nenda usiku pamoja na walioamini miongoni mwa Wana wa Isrāeli, ili Fir’awn na askari wake, ambao watawafuata nyinyi, wasije wakawafikia kabla ya kufika kwenu baharini.»

Fir’awn akawatuma askari wake, alipopata habari kwamba Wana wa Isrāeli wameondoka usiku, (akawaamrisha) wakusanye jeshi lake kutoka miji ya utawala wake.

Fir’awn akasema, «Kwa Hakika, Wana wa Isrāeli waliokimbia pamoja na Mūsā ni pote twevu (ni kundi dhalili) lenye idadi ndogo.

Na wao wamevijaza hasira vifua vyetu kwa kuwa wameenda kinyume na dini yetu na wametoka bila ya idhini yetu,

na sisi sote tuko macho, tuko tayari nao.»

Mwenyezi Mungu Akamtoa Fir’awn na watu wake kwenye ardhi ya Misri yenye mabustani, mabubujiko ya maji, (chemchem)

hazina za mali na majumba mazuri.

Na kama tulivyowatoa, tuliwapatia nyumba hizo Wana wa Isrāeli baada yao wao.

Hivyo basi Fir’awn na askari wake walimfuata Mūsā na waliokuwa pamoja naye wakati wa kuchomoza jua.

Yalipoonana makundi mawili, watu wa Mūsā walisema, «Kwa hakika kikosi cha Fir’auni kimetufikia na kitatuangamiza.»

Mūsā alisema kuwaambia, «Sivyo! Mambo si kama mlivyosema!. Hamtafikiwa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Yuko na mimi kwa msaada, Ataniongoza njia ya kuokoka mimi na kuokoka nyinyi.»

Hapo tukampelekea wahyi Mūsā kwamba, «Piga bahari kwa fimbo yako!» Akapiga. Na bahari ikapasuka njia kumi na mbili kwa idadi ya kabila za Wana wa Isrāeli. Na kila kipande kilichojitenga na bahari ni kama jabali kubwa.

Na tulimsogeza karibu Fir’auni na watu wake mpaka wakaingia baharini.

Na tukamuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja naye wote. Bahari ikaendelea kuachana kwake (kwa ule mpasuko) mpaka wakavuka kwenye nchi kavu.

Kisha tukamzamisha Fir’auni na waliokuwa pamoja naye kwa kuifanya bahari iwafunike baada ya wao kuingia ndani wakimfuata Mūsā na watu wake.

Kwa hakika, katika hilo lililotokea pana mazingatio ya ajabu yenye kuonyesha dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Na wengi wa wafuasi wa Fir’auni hawakuwa ni wenye kuamini, pamoja na alama hii yenye kushinda.

Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi katika kuwatesa waliomkanusha na wakaenda kinyume na amri Yake, Mwenye rehema kwa waja Wake walioamini”.

[Suratu Shuarai 23-67]

Basi alipofikwa firauni na Gharika alisema: Nimeamini kuwa yeye Mwenyezi Mungu hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yule amabaye wamemuamini wana wa Israeli, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Je, sasa hivi, ewe Fir’aun, wakati kifo kimekushukia ndipo, unakubali kuwa wewe ni mja wa Mwenyezi Mungu na hali ulimuasi na ukawa ni miongoni mwa waharibifu wenye kuzuia njia Yake kabla ya adhabu Yake kukushukia! Basi toba haitokunufaisha wakati wa kukata roho na kushuhudia kifo na adhabu”.

“Basi leo tutakuokoa kwa (kuuweka) mwili wako, akutazame mwenye kukanusha kuangamia kwako, ili uwe ni mazingatio kwa watu wenye kuja baada yako kuwaidhika na wewe. Na hakika wengi zaidi kati ya watu ni wenye kughafilika na hoja zetu na dalili zetu, hawazifikirii wala hawazizingatii”.

Na Mwenyezi Mungu akawarithisha watu wa Mussa ambao walikuwa wananyanyaswa, akawarithisha ardhi kuanzia mashariki mpaka magharibi ardhi ambayo aliibariki na vilivyomo ndani yake, na akaangamiza yote aliyoyatengeneza Fir’auni na watu wake na majumba ya kifahari ambayo walikuwa wakiyajenga.

Na akateremsha Mwenyezi Mungu baada ya hapo kwa Mussa kitabu cha Taurati, ndani yake kinaweka wazi halali na haramu ambayo inapasa kwa wana wa Israeli (watu wa Musa) kuifuata.

Kisha Musa akafa -Amani iwe juu yake- na akatuma Mwenyezi Mungu baada yake mitume wengi kwa watu wake -wana wa israeli- wakiwafahamisha njia sahihi kila alipokufa mtume alikuja baada yake Mtume mwingine.

Mwenyezi Mungu alitusimulia visa vya baadhi yao kwa mfano Daudi na Sulaiman na Ayoub na Zakaria, na hakutusimulia sana visa vyao, kisha akamalizia kuwatuma hawa mitume kwa kumtuma Issa mwana wa Maryam juu yake amani, ambaye maisha yake yalikuwa yamejaa alama za utume kuanzia kuzaliwa kwake mpaka kuinuliwa kwake mbinguni.

Baada ya kupita vizazi na vizazi, ilipatwa Taurati aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mussa mabadiliko na kupindishwa kupitia mikono ya mayahudi ambao wanadai kuwa wao ni wafuasi wa Mussa -juu yake amani- Na Mussa yuko mbali nao, na Taurati iliyoko mikononi mwao haihesabiki kuwa ndiyo taurati ambayo iliteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa wameingiza humo mambo ambayo hayastahiki kuwa yametoka kwa Mwenyezi Mungu, na wakamsifia Mwenyezi Mungu katika taurati hiyo kwa sifa ambazo zina mapungufu na ujinga na udhaifu- Ametukuka Mwenyezi Mungu kwa hayo wanayoyasema kutukuka kwa hali ya juu kabisa – amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kutaja sifa zao:

“Maangamivu na onyo kali kwa wanavyuoni wa shari wa Kiyahudi ambao wanaandika kitabu kwa mikono yao kisha wanasema, “Hiki kinatoka kwa Mwenyezi Mungu.” Nacho kinaenda kinyume na yale ambayo Mwenyezi Mungu Amemteremshia Nabii wake Mūsā rehema na amani zimshukie, ili wapokee, kwa kitendo hicho, manufaa ya ulimwenguni. Basi wao watapata mateso yenye kuangamiza kwa sababu ya kuuandika kwao ubatilifu huu kwa mikono yao, na watapata mateso yenye kuangamiza kwa sababu ya mali ya haramu wanayoichukua kwa shughuli yao hiyo, kama hongo na mfano wake.

[Suratul Baqara 79]

About The Author