J- Mtume Shuaibu -Amani iwe juu yake.
Kisha akatuma Mwenyezi Mungu baada ya hapo kwa watu wa Madyan ndugu yao Shuaibu baada ya kuwa wamepotea na wakaachana na uongofu, na ikaenea tabia mbovu ya kuwafanyia watu uadui na kupunguza katika kilo na mizani, basi akatuhabarisha Mwenyezi Mungu kuhusu watu hao kwa maneno yake aliposema:
“Hakika tulimtuma, kwa watu wa kabila linalokaa Madyan, ndugu yao Shu’ayb, amani imshukie, akasema kuwaambia, «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika. Hamna Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu. Mtakasieni ibada. Hakika imewajia nyinyi hoja, kutoka kwa Mola wenu, juu ya ukweli wa yale ninayowaitia. Watekelezeeni watu haki zao kwa kutimiza vipimo na mizani. Na msiwapunguzie haki zao mkawadhulumu. Wala msifanye uharibifu katika ardhi, kwa ukafiri na kudhulumu, baada ya kuwa imetengenezwa kwa sheria za Mitume waliopita, amani iwashukie. Hayo niliyowaitia nyinyi ni bora kwenu katika ulimwengu wenu na Akhera yenu, iwapo nyinyi ni wenye kuniamini katika yale ninayowaitia, ni wenye kuzifuata sheria za Mwenyezi Mungu kivitendo”.
«Na wala msikae katika kila njia mkiwatisha watu kwa kuwaua wasipowapa mali yao, mkimzuia aliyemuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, na akatenda mema asifuate njia iliyonyooka, na mkataka njia ya Mwenyezi Mungu iwe kombo, na mnaipotoa mkifuata matamanio yenu, na mnawafukuza watu wasiifuate. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, juu yenu ilipokuwa idadi yenu ni chache Mwenyezi Mungu akawafanya muwe wengi mkawa mna nguvu, wenye enzi. Na angalieni, ulikuwa vipi mwisho wa wale waharibifu katika ardhi na ni yapi yaliyowashukia ya maangamivu na kuvunjikiwa?
Na iwapo kundi miongoni mwenu waliyakubali yale Aliyonituma nayo Mwenyezi Mungu na kundi la watu wengine wasiyakubali hayo, basi ngojeni, enyi wakanushaji wa hukumu ya Mwenyezi Mungu inayotoa uamuzi baina yetu na nyinyi, itakapowashukia adhabu Yake ambayo aliwaonya nayo. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, ni mbora wa wenye kuhukumu baina ya waja Wake.
Walisema watukufu na wakubwa wa watu wa Shu’ayb waliokataa, kwa kiburi, kumuamini Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume Wake Shu’ayb, amani imshukiye, «Tutakutoa, ewe Shu’ayb, wewe na walio pamoja na wewe kutoka kwenye miji yetu, isipokuwa ukiwa utarudi kwenye dini yetu.» Shu’ayb akasema akilipinga na kulionea ajabu neno lao, «Je, tuwafuate nyinyi kwenye dini yenu na mila yenu ya batili hata kama sisi tunaichukia kwa kujua kwetu ubatili wake?»
Akasema Shu’ayb kuwaambia watu wake, kwa kuongezea, «Tutakuwa tumemzulia Mwenyezi Mungu uongo tukirudi kwenye dini yenu baada ya Mwenyezi Mungu kutuokoa nayo. Haiwezekani kwetu kugeuka kuifuata dini isiyokuwa ya Mola wetu, isipokuwa iwapo Mwenyezi Mungu, Mola wetu, Ametaka. Hakika Mola wetu Amekiendea kila kitu kwa ujuzi, kwa hivyo Anakijua kinachowafaa waja. Ni kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, mategemeo yetu ya kupata uongofu na ushindi. Ewe Mola wetu, toa uamuzi wa haki kati yetu na watu wetu, na wewe ndiye mbora wa wenye kutoa uamuzi.
Wakasema watukufu na wakubwa wenye kukanusha, wenye kupinga ulinganizi wa Tawhīd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) waliofikia kiwango cha juu katika ujeuri na uasi, wakitahadharisha kwamba Shu’ayb asifuatwe, «Kwa hakika, lau mnamfuata Shu’ayb, nyinyi kwa hivyo mtakuwa wenye kuangamia.»
Basi wale waliokufuru walishikwa na tetemeko kali ambalo lilizitoa nyoyo zao, wakawa wameangamia katika mji wao, wamegandama na ardhi kwa magoti yao na nyuso zao, hakuna yeyote kati yao aliyeponyoka.
Wale ambao walimkanusha Shu’ayb walikuwa kana kwamba hawakukaa kwenye nyumba zao wala hawakustarehe humo. Kwani walimalizwa, isibaki alama yoyote yao, wakapata hasara na maangamivu duniani na Akhera.
Shu’ayb alijiepusha nao, alipokuwa na yakini kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuwashukia, na akasema, «Enyi watu wangu, ‘Nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nimewashauri muingie kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu na muache hayo mliyonayo; hamkusikia wala hamkutii. Vipi mimi niwasikitikie watu walioukataa upweke wa Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake?’»
[Suratul Aaraf 85-95]