Dini ya Uislamu

Inatangazwa kupitia Dalili zitokanazo na Qur'ani na Sunnah za Mbora wa Viumbe.

J- Mtume Ibrahim -Amani iwe juu yake.

Kisha akamtuma Mwenyezi Mungu baada ya hapo Nabii Ibrahim – juu yake amani- kwa watu wake baada ya kuwa wamepotea na ni wenye kuabudu Sayari na masanamu, Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Kwa hakika, tulimpa Ibrāhīm uongofu wake ambao yeye aliwalingania watu waufuate kabla ya Mūsā na Hārūn. Na sisi tulikuwa tunajua kwamba yeye anastahiki hilo.

Pindi aliposema kumwambia baba yake na watu wake, «Ni masanamu gani hawa mliowatengeneza kisha mkakaa kuwaabudu na mkajilazimisha nao.»

Wakasema, «Tuliwakuta baba zetu wakiwaabudu, na sisi tunawaabudu kwa kuwaiga wao.»

Ibrāhīm akawaambia, «Kwa hakika nyinyi na wazee wenu, kwa kuwaabudu kwenu hawa masanamu, mko mbali waziwazi na haki.»

Wakasema, «Je, neno hili ambalo umekuja nalo kwetu ni la usawa na ukweli, au neno lako ni la mtu anayefanya mzaha na shere, hajui analosema?»

Ibrāhīm, rehema na amani zimshukie, akasema, «Bali Mola wenu Ambaye ninawalingania mumuabudu Ndiye Mola wa mbingu na ardhi Ambaye Ameziumba, na mimi ni mwenye kulitolea ushahidi hilo.

«Na ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, nitawachimba masanamu wenu niwavunjevunje baada ya nyinyi kuondoka kwenda zenu na kuwaacha.»

“Hapo Ibrāhīm akawavunjavunja masanamu akawafanya vipande- vipande vidogo na akamuacha mkubwa wao, ili watu wake wapate kumrudia kumuuliza, na ili uelemevu wao na upotevu wao upate kujulikana waziwazi, na ili hoja isimame kwao”.

“Na watu wakarudi na wakawaona masanamu wao wamevunjwa- vunjwa na wametwezwa (wamedhalilishwa). Hapo wakaulizana wao kwa wao, «Ni nani aliyefanya haya kwa waungu wetu? Huyo, kwa kweli, ni dhalimu kwa kuwa na ujasiri juu ya waungu wanaostahiki kuheshimiwa na kutukuzwa.»

Hapo wale waliomsikia Ibraim akiapa kwamba atawachimba masanamu wao, «Tulimsikia kijana akiwataja kwa ubaya, anaitwa Ibrāhīm.»

Viongozi wao wakasema, «Mleteni Ibrāhīm mbele ya watu aonekane, wapate kushuhudia kukubali kwake makosa ya aliyoyasema, ili iwe ni hoja dhidi yake.»

Ibrāhīm akaletwa, na wakamuuliza kwa njia ya kumpinga, «Je, ni wewe uliowavunjavunja waungu wetu?» Wakikusudia masanamu wao.

Ibrāhīm akalipata alitakalo la kuonyesha wazi upumbavu wao na huku wakiona, akasema, «Aliyewavunjavunja ni huyu sanamu mkubwa, waulizeni hilo waungu wenu mnaowadai iwapo watasema au watawapa majibu.»

“Hapo wakatahayari na ukawafunukia wazi upotevu wao, vipi wanawaabudu na ilhali wao wanashindwa kujitetea wenyewe kitu chochote wala kumjibu mwenye kuwauliza? Na wakakubali wenyewe kuwa wamefanya udhalimu na ushirikina”.

“Punde si punde ukakamavu wao uliwarudia baada ya kushindwa hoja, wakageuka kurudi kwenye ubatilifu wao na wakatumia hoja dhidi ya Ibrāhīm ambayo ni hoja dhidi yao wakasema, «Vipi tutawauliza na hali wewe unajua kuwa hawa hawasemi?»

“Ibrāhīm akasema: «Vipi mnaabudu masanamu wasionufaisha wanapoabudiwa wala kudhuru wanapoachwa?

“Ubaya ni wenu na ni wa waungu wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Kwani hamtii akili mkajua uovu wa haya mliyonayo?»

Ilipoporomoka hoja yao na ukweli ukajitokeza, waliamua kutumia uwezo wao na wakasema, «Mchomeni Ibrāhīm kwa moto mkionyesha hasira kwa ajili ya waungu wenu, iwapo nyinyi ni wenye kuwasaidia basi washeni moto mkubwa na mumtupe ndani yake.»

Mwenyezi Mungu Akamsaidia Mtume Wake na Akauambia moto, «Kuwa baridi na salama kwa Ibrāhīm!» Ili asipatwe na udhia wala asifikwe na jambo la kuchukiza.

“Na wale watu walimtakia Ibrāhīm maangamivu na Mwenyezi Mungu Akavitengua vitimbi vyao na Akawafanya wao wawe ni wenye kushindwa na kuwa chini”.

[Surat Al-anbiyaa 50-70]

Kisha akahama Ibrahim -Amani iwe juu yake- na mwanaye baada ya hapo kutoka Palestina mpaka Makkah, na akamuamrisha Mwenyezi Mungu Ibrahim na Mwanaye kujenga Al-kaaba tukufu, na akawaita watu kuja kuhiji katika nyumba hiyo na kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake.

“Na tulimuusia Ibrahim na mwanaye Ismail yakuwa waisafishe nyumba yangu kwa wenye kuizunguka na wenye kukaa humo na wenye kurukuu na kusujudu”

[Al Baqarah: 125]

About The Author