H- Mtume Isa Amani iwe juu yake.
Kwa hakika alikuwa Maryamu mwana wa Imrani Bikira aliyekuwa twahara ni mshika ibada miongoni mwa washika ibada na mwenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu zilizoteremshwa kwa Mitume baada ya Musa, na alikuwa ni katika familia aliyoichagua Mwenyezi Mungu kwa walimwengu wa wakati huo. kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“Hakika Mwenyezi Mungu Amemchagua Ādam, na Nuhu, na jamii ya Ibrāhīm na jamii ya ‘Imrān Akawafanya kuwa bora kwa watu wa zama zao”.
[Al Imran: 33].
Na wakampa habari njema Malaika kwa kuchaguliwa kwake na Mwenyezi Mungu.
“Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Malaika waliposema, «Ewe Maryam, hakika Mola wako Amekuchagua kwa kumtii na Amekusafisha na tabia duni na Amekuchagua kati ya wanawake wa ulimwengu wote katika zama zako.
«Ewe Maryam, Endelea daima kumtii Mola wako, simama kwa utulivu na unyenyekevu na usujudu na urukuu pamoja na wenye kurukuu kwa kumshukuru Mola wako juu ya neema Alizokutunukia.»
[Surat Al-imran 42-43].
Kisha akatoa habari Mwenyezi Mungu kutakasika na machafu ni kwake na mtukufu, Namna gani alivyomuumba Issa katika kizazi chake pasi na yakuwa na Baba. Kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“Na utaje, ewe Mtume, katika Qur’ani hii habari ya Maryam alipojiweka mbali na watu wake, akajifanyia mahali upande wa Mashariki kando na wao.
Akaweka kizuizi chenye kumsitiri na jamaa zake na watu wengine, hapo tukampelekea Malaika Jibrili akajitokeza kwake katika sura ya binadamu aliyetimia umbo.
Maryam akasema kumwambia, «Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu aniepushe nawe usinifanyie ubaya, iwapo wewe ni miongoni mwa wanaomcha Mwenyezi Mungu.»
Malaika akamwambia, «Kwa hakika, mimi ni mjumbe wa Mola wako, Amenituma kwako nikutunuku mtoto wa kiume aliyesafika na madhambi.»
Maryam akamwambia Malaika, «Vipi mimi niwe na mtoto wa kiume, na hakuna binadamu aliyenigusa kwa ndoa ya halali, na mimi sikuwa mzinifu?»
Malaika akasema kumwambia, «Mambo ni hivyo kama unavyoeleza kwamba hakuna binadamu aliyekugusa na hukuwa mzinifu, lakini Mola wako Amesema, ‘Jambo hili kwangu ni jepesi, na ili mtoto huyu awe ni alama kwa watu yenye kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na awe ni rehema itakayotokana na sisi kwake yeye, kwa mama yake na kwa watu.’» Na kupatikana kwa Īṣsā kwa namna hii lilikuwa ni jambo lililokadiriwa katika Ubao uliohifadhiwa, basi hapana budi lifanyike.
Maryam akabeba mimba ya mtoto wa kiume baada ya Jibrili kupuliza kwenye mwanya wa kanzu yake, na pulizo hilo likafika kwenye uzao wake, na kwa sababu hiyo mimba ikaingia, na akaenda nayo mahali pa mbali na watu.
Na uchungu wa mimba ukamfanya aende kwenye kigogo cha mtende, hapo akasema, «Natamani kama ningelikufa kabla ya siku ya leo na nikawa kitu kisichojulikana, kisichotajwa na kisichotambulika ‘ni nani mimi?.’»
Jibrili au ‘Īssā akamwita na kumwambia, «usisikitike, kwani Mola wako amekufanyia chini yako mkondo wa maji.
«Na ukitikise kigogo cha mtende, zitakuangukia tende mbivu laini zitokazo mtini.
«Basi zile tende hizo mbivu na unywe maji na ujifurahishe kwa huyo mtoto mwenye kuzaliwa. Na umuonapo yeyote miongoni mwa watu, akakuuliza juu ya jambo lako, mwambie, ‘Mimi nimejilazimisha nafsi yangu kwa Mwenyezi Mungu ninyamaze, sitasema na mtu leo.’» Kunyamaza kimya kulikuwa ni ibada katika Sheria yao, na haikuwa hivyo katika Sheria ya Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Hapo Maryam aliwajia watu wake, naye amembeba mtoto wake, akitokea mahali pa mbali. Walipomuona namna hiyo, walisema kumwambia, «Ewe Maryam! Umeleta jambo kubwa ulilolizua.
«Ewe dada ya mtu mwema Hārūn! Baba yako hakuwa ni mtu mbaya anayefanya machafu, na mama yako hakuwa ni mwanamke mbaya anayefanya umalaya.»
Maryam akaashiria kwa mwanawe Īssā ili wamuulize na waseme naye. Wakasema kwa kumpinga, «Vipi tutasema na ambaye bado yuko mlezini (katika mbeleko) tena mchanga wa kunyonya?»
Īssā akasema, naye akiwa katika hali ya uchanga wa kuwa mlezini akinyonya, «Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, Ameamua kunipatia Kitabu, nacho ni Injili, na amenifanya kuwa Nabii.
«Na Amenifanya niwe na wingi wa wema na manufaa popote nipatikanapo, na ameniusia kutunza Swala na kutoa Zaka muda wote nitapokuwa hai.
«Na Amenifanya mimi niwe mwenye kumtendea wema mama yangu, na hakunifanya ni mwenye kujiona wala ni mbaya mwenye kumuasi Mola wangu.
«Na salamu na amani ziko juu yangu mimi siku niliyozaliwa, siku nitakapokufa na siku nitakapofufuliwa nikiwa hai siku ya Kiyama.»
Huyo tuliyokuhadithia, ewe Mtume, sifa zake na habari zake ndiye Īssā mwana wa Maryam pasina shaka, hali ya kuwa yeye ni neno la haki ambalo Mayahudi na Manaswara wanalitia shaka.
Haikuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wala hainasibiani na Yeye kujichukulia mtoto miongoni mwa waja wake na viumbe vyake, Ameepukana na kutakasika na hilo; Akiamua jambo lolote, miongoni mwa mambo, na Akalitaka liwe, dogo au kubwa, halimkatalii, kwa hakika Yeye huliambia, «Kuwa» na likawa kama alivyolitaka liwe.
Na Īssā aliwaambia watu wake, «Na hakika ya Mwenyezi Mungu, Ambaye nawalingania nyinyi Kwake, ni Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni Yeye Peke Yake Asiye na mshirika, kwani mimi na nyinyi tuko sawa katika uja na kumnyenyekea Yeye. Hii ndio njia iliyonyooka”.
[Surat Maryam 16-36]
Na Issa -Amani iwe juu yake- alipowalingania watu kumuabudu Mwenyezi Mungu, kuna waliomuitikia na kuna wengi walio kataa ulinganiaji wake, na akaendelea na ulinganiaji wake akiwalingania watu kwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu lakini wengi walimkufuru na kumfanyia uadui na wakajaribu kumuua! akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kumwambia Issa:
(Ewe Issa hakika mimi nitakutimizia muda wako na nitakunyanyua kukuleta kwangu na nitakutwaharisha kuepukana na wale waliokufuru)
[Al-Imran: 55].
Basi Mwenyezi Mungu akauweka mfanano kwa mmoja wa waliokuwa wakimfukuza wakamshika wakidhani kuwa ndiyo Issa bin Maryam -juu yake amani- wakamuuwa na wakamsulubu, na ama Mtume Issa bin Maryam kwa hakika Mwenyezi Mungu alimuinua kumpeleka kwake. Na kabla ya kuihama dunia aliwapa bishara watu wake kuwa Mwenyezi Mungu atamtuma Mtume mwingine jina lake anaitwa Ahmad ataieneza Mwenyezi Mungu dini hiii kupitia kwake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“Wakumbushe ewe Mtume, watu wako pindi Īssā, mwana wa Maryam, alipowaambia watu wake, «Mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu, ni mwenye kusadikisha Taurati iliyokuja kabla yangu na ni mwenye kushuhudilia ukweli wa Mtume atakayekuja baada yangu, jina lake ni Ahmad, naye ni Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani,na ni mwenye kulingania watu wamuamini, basi alipowajia Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani, kwa aya zilizo wazi walisema, «Huu ni uchawi waziwazi.»
[Surat swaffi 6]
Kisha ukapita muda wa miaka kadhaa, katika zama hizo wakagawanyika wafuasi wa Nabii Issa na likatoka kundi miongoni mwao wakapituka mipaka na wakadai yakuwa Issa ni mwana wa Mungu -Ametakasika Mwenyezi Mungu kwa yale wayasemayo kutakasika kuliko kukubwa- walidanganyika kwa hilo kwakuwa walimuona Issa ni mtoto asiyekuwa na baba, basi akatoa habari Mwenyezi Mungu kuhusu hilo kwa kauli yake:
“Hakika mfano wa Mwenyezi Mungu kumuumba ‘Īssa, bila ya baba, ni kama mfano wa Mwenyezi Mungu kumuumba Adam, bila ya baba wala mama. Mwenyezi Mungu Alimuumba kutokana na mchanga wa ardhi kisha Akamwabia, «kuwa kiumbe», akawa. Basi madai ya uungu wa ‘Īssā kwa kuwa aliumbwa bila ya baba, ni madai ya uongo. Ādam, amani imshukie, aliumbwa bila ya baba wala mama, na wote wamekubaliana kwamba yeye ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu.
[Al Imran: 59].
Wala kuumbwa kwa Issa bila baba si jambo la ajabu sana kuliko kuumbwa kwa Adam pasina kuwa na baba wala mama.
Na kwa ajili hiyo basi Mwenyezi Mungu anawasemesha wana wa Israeli katika Qur’ani ili wajiweke mbali na kukufuru, hii kwa maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:
“Enyi watu wa Injili! Msiikiuke itikadi ya haki katika dini yenu, na msiseme kuhusu Mwenyezi Mungu isipokuwa haki. Hivyo basi, msimfanye kuwa Ana mke wala msimfanye kuwa ana mwana; hakika Al-Masīḥ ‘Īssā, mwana wa Maryam, ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Amemtuma kwa haki na Amemuumba kwa neno ambalo Amemtuma nalo Jibrili alipeleke kwa Maryam, nalo ni neno Lake, «Kuwa!» na ikawa. Nalo ni mvivio (mpulizo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, aliouvivia Jibrili kwa amri ya Mola Wake. Kwa hivyo , aminini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja na mjisalimishe Kwake na muwaamini Mitume Wake katika yale waliowaletea kutoka kwa Mwenyezi Mungu na muyafuate kivitendo. Wala msimfanye ‘Īssā na mama yake kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Komeni na matamshi hayo! Itakuwa bora kwenu kuliko hayo mliyonayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola Mmoja, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Vilivyoko mbinguni na ardhini ni miliki Yake. Basi vipi Atakuwa na mke au mtoto kati ya hivyo? Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wa kupanga mambo ya viumbe Wake na kuendesha maisha yao. Hivyo basi, mtegemeeni, Yeye Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Mwenye kuwatosha”.
Hatoona unyonge Issa kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu.Vile vile Malaika waliokaribishwa kukubali kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Na yeyote mwenye kuona unyonge kufuata kikamilifu na kunyenyekea na akafanya kiburi, Basi hao Mwenyezi Mungu Atawafufua Awakusanye Kwake Siku ya Kiyama, Atoe uamuzi baina yao kwa hukumu Yake ya uadilifu na Amlipe kila mmoja kwa kile anachostahili.
Ama wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu, kiitikadi, kimaneno na kivitendo, wakasimama imara kufuata sheria Zake, basi Yeye Atawalipa thawabu za vitendo vyao na Atawaongeza kutokana na fadhila Zake. Na ama waliokataa kumtii Mwenyezi Mungu na wakafanya kiburi kwa kutojidhalilisha Kwake, Atawaadhibu adhabu iumizayo. Hawatompata wa kuwasimamia atakayewaokoa na adhabu Yake, wala wa kuwanusuru ambaye atawanusuru badala ya Mwenyezi Mungu”.
[Surat Nisaai 171- 173]
Na atamsemesha Mwenyezi Mungu Nabii Issa siku ya Kiyama kwa kauli yake :
Na kumbuka pindi atakaposema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Siku ya Kiyama, «Ewe ‘Īssā mwana wa Maryam! Kwani wewe uliwaambia watu, ‘nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni waabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu’?» ‘Īssā atajibu, kwa kumtakasa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kumuepusha na sifa za upungufu, «Haipasii kwangu kuwaambia watu yasiyokuwa haki. Nikiwa nililisema hili, basi ushalijua. Kwani hakuna chochote kinachofichikana kwako. Wewe unayajua yaliyomo ndani ya nafsi yangu, na mimi siyajui yaliyomo ndani ya nafsi yako. Hakika yako wewe Ndiye Mjuzi wa kila kitu, kilichofichikana au kuwa wazi.»
‘Īssā, amani imshukie, atasema, «Ewe Mola wangu! Sikuwaambia wao isipokuwa yale uliyonitumia wahyi nayo na ukaniamrisha kuyafikisha, ya kukupwekesha wewe tu na kukuabudu. Na mimi nilikuwa nikishuhudia vitendo vyao na maneno yao nilipokuwa nikiishi nao. Na uliponikamilishia muda wangu wa kuishi katika ardhi, ukanipaza mbinguni nikiwa hai, ulikuwa wewe ndiye Mwenye kuzichungulia siri zao, na wewe ni Mwenye kushuhudia kila kitu, hakifichiki kwako chochote chenye kufichika ardhini au mbinguni”.
“Hakika yako wewe , ewe Mwenyezi Mungu, ukiwa utawaadhibu, basi wao ni waja wako, na wewe ndiye Mjuzi wa hali zao, unawafanya unavyotaka kwa uadilifu wako. Na ukiwa utawasamehe, kwa rehema yako, wale waliofuata njia za kuwafanya wasamehewe, basi wewe ndiye Mshindi Asiyeshindwa, Mwenye hekima katika uendeshaji wa mambo yake na amri Zake”. Aya hii inamsifu Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa hekima Yake, uadilifu Wake na ukamilifu wa ujuzi Wake.
Mwenyezi Mungu Atamwambia ‘Īssā Siku ya Kiyama, «Hii ndiyo Siku ya Malipo ambayo kutawafaa wale waliompwekesha Mwenyezi Mungu kule kumpwekesha kwao Mola wao na kufuata kwao sheria Yake, ukweli wa nia zao, maneno yao na matendo yao. Watakuwa na mabustani ya Pepo, inayopita mito chini ya majumba yake ya fahari, hali ya kukaa humo milele. Mwenyezi Mungu Ameridhika nao ndipo Akayakubali mema yao, na wao wameridhika naye kwa malipo mazuri mengi aliyowapa. Kwa Malipo hayo na kuwa Yeye Ameridhika nao huko ndiko kufuzu kukubwa.
[Al Maaidah: 116-119].
Kwa hivyo Masihi Issa Mwana wa Mariamu -juu yake amani- yuko mbali na kundi hili la mamilioni ambao wanajiita wenyewe kwa jina la Wakristo na wanaamini kuwa wao ni wafuasi wa Kristo (Masihi).