E- Mtume Saleh -Amani iwe juu yake.
Kisha ukapita muda kidogo, na likaanza kabila la Thamuud kaskazini mwa bara arabu na wakapotea kwa kuacha njia iliyonyooka na wakashika njia ya upotovu wa waliokuwa kabla yao, hivyo akawatumia Mwenyezi Mungu mtume atokanaye na wao ambaye ni (Swalehe) juu yake amani na akamuunga mkono kwa alama zinazo julisha juu ya ukweli wake, nayo ni Ngamia mkubwa asiyekuwa na wakufanana naye katika viumbe, na akatufahamisha Mwenyezi Mungu Mtukufu habari zake akasema:
“Na tulimtuma, kwenda kwa watu wa kabila la Thamūd, ndugu yao Ṣwaleḥ, walipoabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Ṣāleḥ aliwaambia, «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hamna mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, mtakasieni ibada, nimewajia na hoja juu ya ukweli wa yale ninayowaitia kwayo. Nayo ni kuwa nilimuomba Mwenyezi Mungu mbele yenu, Akawatolea kutoka kwenye jiwe hili ngamia mkubwa kama mlivyoomba, basi muacheni ale kwenye malisho yaliyoko kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, na msimfanyie lolote la kumdhuru, mkifanya hivyo, mtapatwa na adhabu iumizayo.
Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, Alipowafanya nyinyi mnashika nafasi za waliokuwa kabla yenu katika ardhi, baada ya kabila la ‘Ād, Akawamakinisha nyinyi katika ardhi nzuri, mkaifanya makao, mkajenga kwenye mabonde yake majumba makubwa na mkayachonga majabali yake ili mfanye majumba mengine. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu na msizunguke katika ardhi kwa uharibifu”.
“Wakasema mabwana na wakubwa wa wale waliokuwa wakijiona kuwa ni wakubwa, miongoni mwa watu wa Ṣāleḥ, kuwaambia wale waliokuwa wakiwafanya wanyonge na kuwadharau, «Kwani mnajua kwamba Ṣāleḥ ametumwa kwetu na Mwenyezi Mungu?» Wale walioamini walisema, «Sisi tunayaamini yale ambayo Mwenyezi Mungu Amemtuma nayo na tunaifuata sheria aliyokuja nayo.
Wakasema wale waliojiona, «Sisi ni wenye kuyakanusha hayo mliyoyaamini nyinyi na kuyafuata kuhusu unabii wa Ṣāleḥ.”
Wakamchinja ngamia kwa kutojali onyo la Ṣāleḥ, na wakaingiwa na kiburi kilichowafanya wasifuate amri ya Mola wao na wakasema, kwa kejeli na kwa kuona kuwa adhabu iko mbali na wao, «Ewe Ṣāleḥ, tuletee hiyo adhabu ambayo unatuonya nayo, iwapo wewe ni miongoni mwa Mitume wa Mwenyezi Mungu!»
“Basi wale waliokufuru walishikwa na tetemeko kali ambalo lilizitoa nyoyo zao, wakawa wameangamia katika mji wao, wamegandamana na ardhi kwa magoti yao na nyuso zao, hakuna yeyote kati yao aliyeponyoka”.
“Ṣwalehe, amani imshukie, alijiepusha na watu wake, walipomchinja ngamia, na maangamivu yakawa ni yenye kuwashukia, na akasema kuwaambia, «Enyi watu wangu! Nimewafikishia yale Mola wangu Aliyoniamuru niwafikishie, kuhusu maamrisho Yake na makatazo Yake, na nimewafanyia bidii kiasi nilichoweza katika kuwavutia kwenye kheri na kuwakemea shari na kuwa muaminifu, lakini nyinyi hamuwapendi waaminifu kwenu, ndipo mkayakataa maneno yao na mkamtii kila shetani aliyelaaniwa.»
[surat Aaraf 73-74].
Na akatuma Mwenyezi Mungu baada ya hapo mitume wengi kwa kila Umma hapa duniani, na hakuna Umma wowote isipokuwa alipita katika umma huo mtume, Mwenyezi Mungu alitupa habari ya baadhi yao na wengine wengi hakutupa habari zao na wote hao mitume wametumwa na ujumbe mmoja nao ni kuwaamrisha watu wamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika wake, na kuwacha kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu.
“Kwa hakika tulipeleka kwa kila umma uliopita mjumbe wa kuwaamrisha wao kumuabudu Mwenyezi Mungu na kumtii Peke Yake, na kuacha kumuabudu asiyekuwa Yeye miongoni mwa Mashetani, mizimu, wafu na vinginevyo kati ya vile vinavyotegemewa badala ya Mwenyezi Mungu. Basi wakawa miongoni mwao wale ambao Mwenyezi Mungu aliwaongoa wakafuata njia ya Mitume, na kati yao wakapatikana wakaidi waliofuata njia za upotofu, hapo ikapasa kwao upotevu na Mwenyezi Mungu Asiwaafikie (hakuwawezesha kuongoka). Basi tembeeni katika ardhi na mjionee kwa macho yenu vipi yalivyokuwa marejeo ya hawa wakanushaji na maangamivu yaliyowashukia, mpate kuzingatia?”
[An Nahli: 36].