D- Mtume Huud -Amani iwe juu.
Kisha baada ya muda fulani alituma Mwenyezi Mungu kwenye kabila la Aad katika sehemu iitwayo Ah’qaaf- baada ya kuwa walikuwa wapotofu na wakiabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu- Mwenyezi Mungu aliwatumia mtume miongoni mwao naye ni (Huud) Amani iwe juu yake.
Ametupa habari Mwenyezi Mungu kuhusu hilo kwa kusema:
“Hakika tulimtuma, kwenda kwa watu wa kabila la ‘Ād, ndugu yao Hūd, walipoabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hamna mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, mtakasieni ibada. Je, hamuiogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu na hasira Zake kwenu?»
Wakasema wale viongozi waliokufuru katika watu wa Hūd, «Sisi tunajua kwamba wewe, kwa kutuita sisi kuacha kuabudu waungu wetu na kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ni mpungufu wa akili, na sisi tunaamini kwamba wewe, kwa hayo usemayo, ni katika wale wanaomzulia Mwenyezi Mungu uongo.»
Hūd akasema, «Enyi watu wangu, sina upungufu katika akili yangu, isipokuwa mimi ni mjumbe kutoka kwa Mola wa viumbe wote”.
«Ninawafikishia nyinyi yale ambayo Amenituma nayo Mola wangu kwenu. Na mimi kwenu, katika yale niliyowaita kwayo ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kuitumia sheria Yake, ni mshauri mwenye imani, ni muaminifu juu ya wahyi wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka.
Je, imewafanya nyinyi muone ajabu kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameteremsha kwenu yale ambayo yanawakumbusha mambo yaliyo na kheri kwenu, kwa ulimi wa mtu katika nyinyi, mnaoujua ukoo wake na ukweli wake, ili awaogopeshe adhabu ya Mwenyezi Mungu? Na kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, Alipowafanya nyinyi mshike nafasi ya waliokuwa kabla yenu katika ardhi baada ya kuwaangamiza kaumu ya Nuhu na akawazidishia miili yenu nguvu na ukubwa. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu nyingi juu yenu kwa kutarajia kufanikiwa mafanikio makubwa duniani na Akhera.»
’Ād walisema kumwambia Hūd, amani imshukie, «Je, umetuita tumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na tuihame ibada ya masanamu ambayo tumeirithi kutoka kwa baba zetu? Basi tuletee adhabu ambayo unatutisha nayo iwapo wewe ni miongoni mwa wakweli katika hayo usemayo.»
Hūd alisema kuwaambia watu wake, «Mshashukiwa na adhabu kutoka kwa Mola wenu, Aliyetukuka na kuwa juu, «Mnajadiliana na mimi juu ya masanamu hawa mliowaita waungu, nyinyi na baba zenu? Mwenyezi Mungu Hakuteremsha hoja yoyote wala dalili ya kuwa waabudiwe, kwani wao wameumbwa, Hawadhuru wala hawanufaishi; mwenye kuabudiwa peke yake si mwingine ni Muumba, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Basi ngojeni kuteremkiwa na adhabu, kwani mimi, pamoja na nyinyi, nangojea kuteremka kwake. Huu ni upeo wa kuonya na kutisha.»
“Mwenyezi Mungu akamuokoa Hūd na walioamini pamojanaye kwa rehema kubwa kutoka kwake, Aliyetukuka. Na akawaangamiza makafiri wote miongoni mwa watu wake, Akawavunjavunja mpaka wa mwisho wao. Na wao hawakuwa ni Waumini kwa kuwa walikusanya baina ya kukanusha aya za Mwenyezi Mungu na kuacha kufanya vitendo vyema”.
[Suratiul Aaraf 65-72]
Basi Mwenyezi Mungu akawatumia upepo mfululizo kwa siku nane upepo ambao unabomoa kila kitu kwa amri ya Mola wake, na Mwenyezi Mungu akamuokoa Huud na wale walioamini pamoja naye.