Dini ya Uislamu

Inatangazwa kupitia Dalili zitokanazo na Qur'ani na Sunnah za Mbora wa Viumbe.

C- Nuhu -juu yake Amani.

Kwa hakika ilikuwa tofauti ya miaka kati ya Nuhu na Adamu ni karne kumi, alimtuma Mwenyezi Mungu kwa watu wake baada ya kuwa watu hao wamepotea na wakawa wanaabudu miungu badala ya kumuabudu Mwenyezi Mungu, na wakawa wanaabudu masanamu na mawe na makaburi na katika miungu yao iliyokuwa maarufu zaidi ni Wadda na Suwaa Yaghuutha na Yauuqa na Nasraa,Mwenyezi Mungu akamtuma kwao ili awarudishe kwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, kama alivyotufahamisha hilo Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa maneno yake:

“Hakika tulimtuma Nūḥu kwa watu wake, ili awalinganie kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa pungufu ni Kwake, na kumtakasia ibada, akasema, «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na mumnyenyekee kwa kumtii, nyinyi hamna Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, mtakasieni ibada. Msipofanya na mkasalia katika kuabudu masanamu yenu, hakika mimi nawaogopea msishukiwe na adhabu ya Siku ambayo shida yenu itakuwa kubwa, nayo ni Siku ya Kiyama.»

[Al A’raf: 59].

Na akaendelea kuwalingania watu wake wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa muda mrefu, na hawakumuamini na Nuhu isipokuwa watu wachache na akamuomba Mola wake kwa kusema:

“Nuhu akasema, «Mola wangu! Kwa hakika mimi nimewalingania watu wangu usiku na mchana ili wakuamini wewe na wakutii.

Ulinganizi wangu kwao ili waamini, haukuwaongezea kitu isipokuwa ni kukimbia na kuipa mgongo haki.

Na mimi kila nikiwalingania wao ili wakuamini wewe, ipate kuwa hiyo ni njia ya wewe kuwasamehe dhambi zao, hutia vidole vyao masikioni mwao, ili wasisikie ulinganizi wa haki, na hujifunika nguo zao wasipate kuniona, na hujikita kwenye ukafiri wao na hufanya kiburi sana cha kutoikubali haki.

Kisha mimi nikawalingania wao kwenye Imani waziwazi na sio kwa kujificha.

Kisha nikawatangazia wao ulinganizi kwa sauti kubwa wakati mwingine, na nikafanya kwa siri huo ulinganizi kwa sauti ya chini wakati mwingine.

Ni kawaambia watu wangu, ‘Muombeni Mola wenu msamaha wa dhambi zenu na tubieni Kwake kutokana na ukafiri wenu, hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia miongoni mwa waja wake na akarudia Kwake.’»

Mtakapotubia na mkaomba msamaha, Mwenyezi Mungu Atawateremshia mvua nyingi ya mfululizo,

Ataiongeza mali yenu na pia watoto wenu, Atawafanya muwe na mabustani ya nyinyi kuneemeka kwa matunda yake na uzuri wake, na Atawajaalia nyinyi muwe na mito ambayo mtaitumia kwa kuipatia maji mimea yenu na pia wanyama wenu.

Mnani nyinyi, enyi watu, hamuweki heshima kwa Mwenyezi Mungu?

na hali yeye Amewaumbeni namna (hatua) baada ya namna (hatua)?”

[Surat Nuuh 5- 14]

Na pamoja na juhudi hii endelevu na pupa ya ajabu ya kuwaongoza watu wake, lakini wao walimfanya kuwa muongo na wakamcheza shere na wakampa sifa ya uwendawazimu.

Basi Mwenyezi Mungu akampa wahyi ya kuwa.

“Hawatomuamini Mwenyezi Mungu isipokuwa walioamini kabla ya hapo, «basi usisikitike, ewe Nūḥu juu ya yale waliokuwa wakiyafanya”.

[Surat Huud 36]

Na akamuamrisha kutengeneza safina ambayo itabeba ndani yake kila yule aliyeamini pamoja naye.

“Na Nuhu akawa anatengeneza jahazi, na kila kundi la wakubwa wa watu wake likimpitia, humcheza shere. Nuhu, aliwaambia, «Iwapo nyinyi mnatucheza shere leo, kwa ujinga wenu wa kutojua ukweli wa ahadi ya Mwenyezi Mungu, basi sisi tutawacheza shere nyinyi kesho wakati wa kuzama kama mnavyotucheza shere”.

Mtajua hapo, itakapokuja amri ya Mwenyezi Mungu kwa hilo, ni yupi ambaye itamjia, hapa ulimwenguni, adhabu ya Mwenyezi Mungu yenye kumtweza (kumdhalilisha) na itamshukia huko Akhera, adhabu ya daima isiyokatika.»

Mpaka ilipokuja amri yetu ya kuwaangamiza wao kama tulivyomuahidi Nuhu kwa hilo, na maji yakachimbuka kwa nguvu kutoka kwenye tanuri, mahala pa kuchomea mikate, ikiwa ni alama ya kuja adhabu, tulimuambia Nuhu, «Beba ndani ya jahazi kila aina, miongoni mwa aina za wanyama wa kiume na wa kike, na uwabebe ndani yake watu wa nyumbani kwako, isipokuwa yule aliyetanguliwa na Neno kuwa ataadhibiwa katika wale wasiomuamini Mwenyezi Mungu kama mtoto wake na mke wake, na ubebe ndani yake aliyeamini pamoja na wewe katika watu wako.» Na hakuna aliyeamini pamoja naye isipokuwa wachache ingawa yeye alikaa nao kwa muda mrefu”.

Nuhu alisema kuwaambia walioamini pamoja naye, «Pandeni kwenye jahazi kwa jina la Mwenyezi Mungu. Kwa jina la Mwenyezi Mungu itatembea majini, na kwa jina la Mwenyezi Mungu itafika mwisho wa kwenda kwake na kutia nanga kwake. Hakika Mola wangu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za mwenye kutubia na kurudi Kwake miongoni mwa waja Wake, ni Mwingi wa huruma kwao kwa kutowaadhibu baada ya kutubia.

Nayo ikawa inatembeanao kwenye mawimbi yanayopaa na kwenda juu mpaka yakawa kama majabali kwa urefu wake wa kwenda juu. Hapo Nuhu alimuita mtoto wake wa kiume, ambaye alikuwa yupo mahali kando na amejiepusha na Waumini, akamwambia, «Ewe mwanangu, panda na sisi kwenye jahazi na usiwe pamoja na wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, utakuja kuzama.»

Mtoto wa Nuhu akasema, «Nitakimbilia kwenye jabali nijihifadhi na maji na hilo litanizuia na kuzama. Nuhu akamjibu, «Leo hakuna kitu chenye kuzuia amri ya Mwenyezi Mungu na hukumu Yake iliyoteremka kwa viumbe, ya gharika na maangamivu, isipokuwa yule aliyehurumiwa na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, basi amini na upande jahazini pamoja na sisi.» Hapo mawimbi makubwa yalitenganisha baina ya Nuhu na mwanawe na akawa ni miongoni mwa waliogharikishwa wenye kuangamia”.

“Akasema Mwenyezi Mungu kuiambia ardhi, baada ya watu wa Nuhu kuangamia, «Ewe ardhi! Kunywa maji yako. Na ewe mbingu! Simamisha kunyesha mvua.» Na maji yakapungua na yakanywea, na amri ya Mwenyezi Mungu ikapitishwa ya kuangamia watu wa Nuhu, na jahazi ikaegesha juu jabali la Jūdīy. Na hapo kukasemwa, «Kuwa mbali (na rehema ya Mwenyezi Mungu) ni kwa wale madhalimu waliokiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu na wasiamini.»

Na Nuhu alimlingania Mola Wake kwa kumuomba na akasema, «Mola wangu, wewe umeniahidi kwamba utaniokoa, mimi na jamaa zangu, tusizame na tusiangamie, na hakika mtoto wangu ni miongoni mwa watu wa nyumbani kwangu, na ahadi yako ndio kweli ambayo haibadiliki, na wewe ndiye hodari zaidi wa wenye kuhukumu na muadilifu wao zaidi.»

Mwenyezi Mungu Akasema, «Ewe Nuhu hakika yule mtoto wako aliyeangamia si katika jamaa ambao nilikuahidi kuwa nitawaokoa. Hii ni kwa sababu ya ukafiri wake na kufanya kwake matendo yasiyokuwa mema. Na mimi nakukataza usiniombe jambo usilokuwa na ujuzi nalo. Mimi nakusihi usiwe ni miongoni mwa wajinga kwa kuniomba hilo.»

Akasema Nuhu, «Ewe Mola wangu, Mimi najihami kwako na nataka hifadhi kukuomba kitu nisichokuwa na ujuzi nacho, na usiponisamehe dhambi zangu na ukanihurumia kwa rehema zako, nitakuwa ni miongoni mwa wale waliojinyima hadhi zao na wakaangamia”.

Mwenyezi Mungu Akasema, «Ewe Nuhu Shuka kwenye ardhi kavu kutoka kwenye jahazi, kwa amani na salama zitokazo kwetu, na baraka ikishuka juu yako na juu ya umma katika wale walioko na wewe. Na kuna umma na makundi miongoni mwa watu wa uovu ambao tutawastarehesha katika uhai wa kiulimwengu mpaka ufike muda wao wa kuishi kisha iwapate wao kutoka kwetu adhabu iumizayo Siku ya Kiyama.»

[Surat: 38-48].

About The Author