B- Mtume wa kwanza ni Baba yetu Adam- Amani iwe juu yake-
Amemuumba Mwenyezi Mungu Baba yetu Adamu -juu yake Amani- kutokana na udongo, kisha akampulizia roho itokayo kwake, Amesema Mwenyezi Mungu aliyetukuka jambo lake.
“Na kwa hakika, tumewaneemesha nyinyi kwa kumuumba chanzo chenu – naye ni baba yenu Ādam- kutokana na kutokuwepo kamwe, kisha tukamtia sura ya umbo lake lililo bora kuliko lile la viumbe wengi. Kisha tuliwaamuru Malaika wetu, amani iwashukie, wamsujudie kwa ajili ya kumtukuza na kumuheshimu na kuonyesha ubora wa Ādam. Nao wakamsujudia wote, isipokuwa Ibilisi, ambaye alikuwa pamoja nao, hakuwa ni miongoni mwa wenye kumsujudia Ādam kwa kumuhusudu kwa heshima hii kubwa aliyopewa”.
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Akasema hali ya kumkemea Ibilisi kwa kuacha kwake kumsujudia Ādam, «Ni lipi lililokuzuia usisujudu nilipokuamuru?» Ibilisi akasema, «Mimi ni bora kuliko yeye, kwa kuwa mimi nimeumbwa kwa moto na yeye ameumbwa kwa udongo.» Akaona kuwa moto ni bora kuliko udongo.
“Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia Ibilisi, «Shuka kutoka Peponi, kwani haifai kwako kufanya ujeuri humo; toka Peponi, kwani wewe ni miongoni mwa wanyonge walio madhalili”.
“Ibilisi akasema kumwambia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, alipokata tamaa na rehema Yake, «Nipe muda mpaka Siku ya watu kufufuliwa, ili nipate kumpoteza ninayeweza kumpoteza kati ya wanadamu.»
“Akasema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, «Wewe ni miongoni mwa wale niliowaandikia kucheleweshwa kipindi chao cha kufa mpaka Mvivio (mpulizo) wa Kwanza katika Parapanda pindi viumbe wote watakapokufa.»
(Suratul -Aaraf 10-15)
Na akamuomba Mwenyezi Mungu amcheleweshe na wala asimfanyie haraka kumuadhibu na ampe idhini ya kumpoteza Adamu na kizazi chake kwa husda na kwa kuwachukia, basi Mwenyezi Mungu akamruhusu kwa hekima alizoziona akatawalia shetani upotoshaji wa kumpotosha Adam na kizazi chake isipokuwa waja wake wenyekumtakasia Mwenyezi Mungu ibada, na akamuamrisha Adam na kizazi chake wasimuabudu shetani na wala wasikubali upotoshaji wake na wajilinde kwa Mwenyezi Mungu kutokana na upotoshaji wake, Na ukaanza upotoshaji wa kwanza wa shetani kumpotosha Adam na mke wake Hawa (Ambaye Mwenyezi Mungu alimuumba kutokana na ubavu wake) katika kisa ambacho alikitaja Mwenyezi Mungu -kutakasika na machafu ni kwake.
«Na ewe Ādam, keti wewe pamoja na mke wako Ḥawā’ Peponi na kuleni matunda yaliyo humo popote mnapotaka na wala msile matunda ya mti huu (Aliwatajia mti huo), mkifanya hilo mtakuwa ni madhalimu wenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.»
“Hapo Shetani aliwashawishi Ādam na Ḥawā’ ili awatokomeze kwenye kumuasi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kula matunda ya mti ule ambao Mwenyezi Mungu Aliwakataza kuula, ili mwisho wao uwe ni kufunukwa na tupu zao zilizokuwa zimesitiriwa. Na akawaambia, katika kujaribu kwake kuwafanyia vitimbi, «Hakika Mola wenu Amewakataza kula matunda ya mti huu ili msipate kuwa Malaika na ili msipate kuwa ni miongoni mwa wenye kuishi milele.»
“Na Shetani Aliwaapia Ādam na Ḥawā’ kwa Mwenyezi Mungu kwamba yeye ni miongoni mwa wale wanaowapa nasaha kwa kuwashauri kula kutoka mti ule, huku yeye ni muongo katika hilo”.
“Hapo yeye aliwatia wao ujasiri na akawadanganya wakala kutoka mti huo ambao Mwenyezi Mungu Aliwakataza wasiukaribie. Walipokula kutoka mti huo, ziliwafunuka tupu zao na kikaondoka kile ambacho Mwenyezi Mungu Aliwasitiri nacho kabla ya wao kufanya uhalifu huo, wakawa wanayaambatisha majani ya miti ya Peponi kwenye tupu zao. Hapo Mola wao, Aliyetukuka na kuwa juu, Aliwaita, «Kwani sikuwakataza kula kutoka mti ule na nikawaambia kwamba Shetani, kwenu nyinyi, ni adui ambaye uadui wake uko waziwazi?» Katika aya hii kuna ushahidi kwamba kukaa uchi ni kati ya mambo makubwa na kwamba hilo ni jambo linalochukiza na linaloendelea kuchukiza katika tabia, na ni ovu kwenye akili za watu.
“Ādam na Ḥawā’ walisema, «Ewe Mola wetu, tumejidhulumu nafsi zetu kwa kula kutoka kwenye mti ule. Na iwapo hutatusamehe na kuturehemu, tutakuwa ni miongoni mwa waliopoteza bahati zao katika ulimwengu wao na Akhera yao.» Maneno haya ndiyo yale aliyoyapokea Ādam kutoka kwa Mola wake akayatumia katika kumuomba, ndipo Mola wake Akaikubali toba yake.
“Akasema, Aliyetukuka, kumwambia Ādam, Ḥawā’ na Ibilisi, «Shukeni kutoka mbinguni muende ardhini, baadhi yenu mkiwa ni maadui wa wengine. Huko mtakuwa na mahala pa nyinyi kutulia na pa kujiliwaza mpaka muda wenu ukome.»
“Mwenyezi Mngu, Aliyetukuka, Akasema kumwambia Ādam, Ḥawā’ na kizazi chao, «Huko ardhini mtaishi, yaani mtapitisha siku za uhai wenu duniani, na huko kitakuwa kifo chenu, na kutoka huko Mola wenu atawatoa na awakusanye mkiwa hai Siku ya Ufufuzi.»
“Enyi wanadamu, tumewawekea vazi lenye kusitiri tupu zenu, nalo ni vazi la lazima, na vazi la pambo na kujirembesha, nalo ni vazi la kujikamilisha na kujifurahisha. Na vazi la uchaji Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo, ndilo vazi bora kwa aliyeamini. Hayo Ndiyo ambayo Mwenyezi Mungu Amewaneemesha nayo miongoni mwa alama za umola (ulezi) wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, upweke Wake, wema Wake na rehema Zake kwa waja Wake, ili mpate kuzikumbuka neema hizi na mumshukuru Mwenyezi Mungu juu yake”.
“Enyi wanadamu! Asiwadanganye Shetani akawapambia maasia, kama alivyowapambia wazazi wenu, Ādam na Ḥawā’, akawatoa Peponi kwa sababu hiyo, akawavua vazi lao ambalo Mwenyezi Mungu Aliwasitiri nalo ili tupu zao zifunuke. Shetani na kizazi chake na viumbe wa jinsi yake wanawaona nyinyi, na nyinyi hamuwaoni, basi jichungeni nao. Hakika sisi tumewafanya Mashetani ni wategemewa wa makafiri ambao hawampwekeshi Mwenyezi Mungu wala hawawaamini Mitume Wake wala hawautumii muongozo Wake”.
(Suratul Aaraf 19-27)
Na baada ya kuteremka Adamu Ardhini na akaruzukiwa watoto na kizazi alikufa Adamu – juu yake amani- kisha kikaongezeka kizazi chake taifa baada ya taifa na wakapatwa na upotoshaji wa shetani na akawaenezea tabia ya kwenda kinyume na mafundisho na kuabudu makaburi ya watu wema miongoni mwa baba zao na wakabadilishwa kutoka kwenye imani kupelekwa kwenye shirki, basi Mwenyezi Mungu akawapelekea kwao Mtume naye ni (Nuhu Amani iwe juu yake).